Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume kizigo amesema kuwa katika kuazimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Tanzania imefanikiwa pakubwa kutatua kero za Muungano ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano na kuimarisha ulinzi na usalama kwa Nchi.
Ameyasema hayo wakati akihutubia Katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Muungano yaliyofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo ametaja mafanikio hayo yanatokana na misingi mizuri na Muunganiko walioufanya waasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
"Asili yetu, Babu zetu ni wamoja sisi sote tumeingiliana kidamu, hauwezi kuchagua ndugu ukishazaliwa naye ndugu ni ndugu hata kama haumtaki, undugu wetu ni wadamu na tunapendana hadi Leo Nchi yetu inaadhimisha miaka 58 ya Muungano tumepitia mambo mengi kero za Muungano zimepungua sana sana, tumepiga hatua kubwa ya maendeleo kiuchumi, ulinzi, kiusalama , kijamii na hata kisiasa".Aliongeza Dc Kizigo.
Pamoja na hayo amesema kuwa Matunda ya Muungano yanaonekana Kwa Nchi hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuyaenzi Kwa kufanya kazi kwa bidii , kuendelea kudumisha amani na utulivu ,kuendelea kufuata Sheria za Nchi pamoja na kuendeleza uzalendo ambao uliachwa na waasisi wa Tanzania Kwa kuwa tayari kujitoa kwaajili ya Nchi yao.
Pamoja na hayo aliwataka wananchi kujiandaa na maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 Mwaka huu kwakuwapa ushirikiano wataalamu watakaopita kwenye Kaya zao kwakutoa taarifa muhimu kwani kwakufanya kivyo inapelekea Serikali kuweza kupanga bajeti na kuboresha huduma kwa jamii kwakuainisha vipaumbele mbalimbali kulingana na uhitaji wa jamii.
Awali akiongea katika hafla hiyo Afisa Mazingira Wilaya ya Mkalama Bw. Amon Sanga amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imeungana na watanzania wote kuadhimisha siku hii muhimu Kwa kufanya usafi katika eneo la Halmashauri pamoja na kupanda miti mbalimbali ikiwa ni kuunga mkono juhudi za waasisi hao na kuhakikisha mazingira yanaendelea kutunzwa na kuboreshwa.
Baadhi ya wananchi walihudhuria katika hafla hiyo wameeleza namna wanavyouenzi Muungano kwakufanya kazi kwa bidii Ili kuendelea kupinga Adui wa Maendeleo ambayo ni ujinga , Maradhi na umasikini na kuongeza kuwa Ili kuweza kupambana na hayo yote lazima umoja uwepo baina ya Tanzania bara na Visiwani ili kwapamoja kuweza kuingiliana na kuishi pamoja.
"Mtanzania anayetoka bara akifika Zanzibar ajisikie yupo Tanzania na walio Zanzibar wakifika Tanzania bara wajisikie wapo Tanzania".
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.