Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wameendesha mafunzo kwa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mkalama One, yakilenga kuimarisha uelewa kuhusu afya ya uzazi, usafi wa mwili, haki za mtoto wa kike, na kujitambua.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mkalama, Bi. Experancia Ngelima, aliwasisitiza wanafunzi hao umuhimu wa kutoa taarifa mara wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, iwe shuleni au majumbani.
“Kuna mabinti wanafanyiwa vitu lakini hawasemi. Wengine wanatishiwa, wananyamaza. Tukumbuke, mwisho wa siku ni maisha yako. Ukinyamaza, unaweza kuathirika kisaikolojia na kupata msongo wa mawazo. Ukiwa na jambo, tafuta mtu wa kuzungumza naye,” alisema Bi. Ngelima.
Aidha, Bi. Ngelima aliwakumbusha wanafunzi hao kudumisha usafi wa mwili na mazingira, akibainisha kuwa hatua hiyo husaidia kujikinga na magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uchafu na ukosefu wa huduma bora za usafi hasa kwa wasichana balehe.
Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Mfuko wa Afya Ulioboreshwa (CHF), Bwana Gaffer Venance Mathiacy, alitoa elimu kuhusu manufaa ya kujiunga na mifuko ya bima ya afya ya CHF na NHIF, akieleza namna wanafunzi na familia zao wanavyoweza kunufaika na vifurushi vya huduma za afya vinavyotolewa kupitia mifuko hiyo.
Tukio hilo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kuendelea kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu haki, afya, na ustawi wa mtoto wa kike, sambamba na utekelezaji wa sera za serikali katika kulinda na kuinua hadhi ya mtoto wa kike nchini.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.