Mkalama
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Asia Messos, amewataka vijana waendesha bodaboda wilayani humo kuhakikisha wanatumia vyema mikopo wanayopewa na Halmashauri kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kukuza kipato cha familia zao.
Akizungumza Septemba 24, 2025, wakati wa ziara ya kikazi katika Kijiji cha Nduguti, Kata ya Nduguti, Bi. Messos alikutana na kikundi cha vijana cha Mkombozi, ambacho ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa makundi maalum.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi huyo alitembelea ofisi za kikundi hicho na kukagua shughuli zao za usafirishaji abiria kwa kutumia pikipiki walizonunua kupitia mkopo wa takribani shilingi milioni 25 waliopatiwa na Halmashauri.
“Niwapongeze kwa hatua yenu ya kuungana na kuanzisha kikundi hiki cha ujasiriamali. Naomba sasa mfikirie kufanya makubwa zaidi. Mkirejesha vizuri mkopo huu, Halmashauri ipo tayari kuwapatia hata bajaji,” alisema Bi. Messos.
Aidha, aliwataka vijana hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha vijana wengine kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili nao wanufaike na fursa zinazotolewa na serikali kupitia mifumo ya mikopo isiyo na riba.
Bi. Messos alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kuweka mifumo shirikishi ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya Halmashauri.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.