
Wanawake wa Wilaya ya Mkalama wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia malezi ya watoto ili kuepusha ukatili wa kijinsia katika jamii.Akizungumza Novemba 29,2025 wakati wa mafunzo ya uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake yanayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kupitia mradi wa WILA, Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Singida, Bi. Irene Beichumila, amesema kuwa suala la malezi ni msingi muhimu katika kujenga jamii bora na yenye maadili.

“Tunapokuwa tunatafuta maisha tusisahau suala la malezi ya familia zetu. Tujitahidi kukaa karibu na watoto wetu. Tutenge muda wa kuzungumza nao; kwa kufanya hivyo tutajenga jamii iliyo imara na yenye mwelekeo mzuri,” amesema Bi. Beichumila.
Akiendelea kuhimiza ushiriki wa wanawake katika mafunzo hayo, Bi. Beichumila amewataka washiriki kuzingatia elimu wanayopewa na wataalamu ili kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
“Elimu tunayopata hapa leo tukaifanye kwa vitendo. Twendeni kwa pamoja tukaelimishe wanawake wenzetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumechangia kujikomboa kiuchumi,” amesisitiza.
Mradi wa Uongozi wa Wanawake na Haki za Kiuchumi (WILA) unatekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika Kata za Tumuli na Ibaga, kwa kushirikiana na shirika la UN Women, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kujenga uwezo, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.