Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Sophia Kizigo leo January 11, 2023 amekabidhi vishikwambi 706 kwa Maafisa Elimu, Walimu wa Shule za Sekondari na Msingi ili kurahisisha majukumu yao na kuleta mapinduzi chanya katika Sekta ya Elimu pamoja na kupandisha ufaulu kwa wanafunzi.
Akiongea mapema leo katika makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheketela uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. Kizigo aliwataka kuvitunza na kutumia vishikwambi hivyo katika kupata maarifa mbalimbali ya kielimu na kuwa wabunifu katika kuongeza ufaulu Wilayani.
‘’Walimu hamjawahi kuniangusha leo hii mmepokea vishikwambi hivi nendeni mkavitumie kujitajirisha nyie katika masuala ya Elimu na msiende kupiga picha za wanafunzi na kuwaposti Instagram na sehemu nyingine hiyo itakuwa kinyume na sheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yenu" Aliongeza Mhe. Kizigo
Sambamba na zoezi la ugawaji wa Vishkwambi Mhe. Kizigo aliwataka Walimu kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku pamoja na kuwahamasisha Wazazi kuendelea kupeleka wanafunzi kuripoti shule kwani tayari masomo yamekwishaanza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe.James Mkwega amewasisitiza Walimu kutunza Vishikwambi ili viweze kudumu kwa muda mrefu kwani ni moja ya njia ya mapinduzi ya kidigitali katika Sekta ya Elimu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Asia Messos aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta Vishikwambi ambayo ni ahadi ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kugawa Vishikwambi katika Wilaya zote nchini ili kutoa motisha kwa Walimu katika kutekeleza majukumu yao. Pia alisisitiza kuwa Vishikwambi ni mali ya Serikali na taratibu zote za uwekaji wa kumbukumbu wa vifaa vya Serikali umefuatwa na zoezi hili la ugawaji linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15/01/2023.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.