Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mheshimiwa Moses Machali, amewataka watoto kutumia siku ya Mtoto wa Afrika kama jukwaa la kupinga unyanyasaji na ukatili dhidi yao kwa kuibua na kufichua vitendo hivyo katika jamii wanazoishi, huku wakilenga kufikia ndoto zao za kupata elimu bora.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika katika Kijiji cha Msingi, Kata ya Msingi, Mhe. Machali aliwakumbusha watoto kuwa historia ya siku hii ina asili yake katika tukio la kihistoria lililotokea mwaka 1976 katika Kitongoji cha Soweto, Afrika Kusini, ambapo watoto walinyanyaswa na kupigwa risasi na serikali ya kibaguzi ya Makaburu kwa kudai haki yao ya kupata elimu bora.
“Leo ni siku yenu watoto. Ni siku ya kumthamini mtoto wa Bara la Afrika, siku ya kumjali mtoto na kukumbushana kuwa mtoto anastahili heshima, ulinzi na upendo. Mtoto ni binadamu anayestahili kuishi bila unyanyasaji wa aina yoyote,” alisema Mhe. Machali.
Aidha, aliwahimiza watoto kupendana, kuthaminiana na kuheshimiana kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari ili kutimiza malengo yao ya kielimu. Alisisitiza kuwa watoto wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya mimba za utotoni, ajira hatarishi na vitendo vya unyanyasaji, huku akiwahimiza kuwa jasiri katika kutoa taarifa kuhusu watu wanaowafanyia ukatili.
“Serikali imeweka miundombinu bora na mazingira rafiki ya kujifunzia. Ni jukumu lenu sasa kuhakikisha mnaitumia fursa hiyo kujilinda, kusoma kwa bidii na kufikia ndoto zenu,” aliongeza.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Machali aliitaka jamii nzima – kuanzia familia, majirani, viongozi wa dini na mashirika – kushirikiana katika kulinda haki na ustawi wa mtoto ili kuijenga jamii salama na yenye matumaini kwa vizazi vijavyo.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu: “HAKI YA MTOTO: TULIPOTOKA, TULIPO NA TUENDAKO”, ikilenga kutafakari hali ya upatikanaji wa haki za watoto tangu sera ya Maendeleo ya Mtoto ilipoanzishwa mwaka 2008 hadi sasa.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.