SERIKALI katika kipindi cha miaka miwili imeupatia Mkoa wa Singida Sh.Bilioni 437.683 sawa na ongezeko la asilimia 252.8 ya Sh.Bilioni 124 zilizotolewa mwaka 2019/2020 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, alisema hayo jana (Julai 23 2023) wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya serikali kuanzia Machi 2021 hadi Juni 2023 kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wa kutoa elimu ya makubaliano ya serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uendeshaji wa bandari uliowashirikisha wananchi kutoka mikoa ya Singida,Dodoma na Tabora.
Alisema katika kipindi hicho utekelezaji wa miradi ya umeme zilitolewa Sh.Bilioni 109.6 ambazo zimewezesha vijiji 341 kati 441 sawa na asilimia 77.32 vimeunganishwa huduma ya umeme wa grid ya Taifa hadi kufikia Machi 2021.
Serukamba alisema katika wateja wapya 19,223 waliounganishiwa umeme ni pamoja na shule 287,visima vya maji 23, viwanda vidogo 76, migodi ya Madini ya dhahabu 5,misikiti 43,makanisa 60,mahakama 2 na vituo vya kibiashara 102.
Kuhusu mpango wa TASAF, alisema hadi kufikia Juni 2023 utekelezaji umefika kwenye vijiji vyote 441 vya Mkoa wa Singida na Mitaa 53 ambapo walengwa wamepokea ruzuku ya masharti na ujira wa ajira za muda Sh.Bilioni 14.317 zilizotolewa na Serikali.
Serukamba alisema katika sekta ya afya kwa kipindi hicho zimetolewa Sh.Bilioni 47.272, Elimu Sh.bilioni 56.223, sekta ya uzalishaji serikali Imetoa Sh.Bilioni 44.386, maji Sh.bilioni 14.635.
Aliongeza kuwa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imesaidia ongezeko la upatikanaji wa maji kutoka asilimia 57.9 mwaka 2020/2021 na kufikia asilimia 67.7 Juni 2023 sawa na wakazi 1,109,220 waishio vijijini.
Alisema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) Mkoa wa Singida uliopewa Sh.Bilioni 52.033 ambazo zimeweza kutumika katika ujenzi wa barabara mbalimbali zenye urefu wa kilometa 1,718.31 zinazohudumiwa na wakala huyo.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji wa bandari, Serukamba alisema wanaopinga uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam ni kutokana na kasi ya kubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo hivyo wanahofu watakosa cha kusema hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Alisema amefanikiwa kuusoma mkataba huo ambapo kipo kifungu ibara ya 14 ambacho hakisemwi na wanaopinga mkataba ambacho kinaeleza kuwa iwapo mwekezaji atashindwa kutekeleza vizuri serikali imepewa mamlaka ya kuvunja mkataba na hawezi kuishtaki mahali popote serikali.
"Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanauchumi anajua nini kifanyike katika kuinua uchumi wa nchi hivyo suala la uwekezaji bandari kinachofanyika ni kutaka kuinua uchumi wa nchi hivyo wanaopinga uwekezaji huo hawaoni mbali," alisema.
Serukamba amesema duniani mambo yamebadilika ili watu waje wawekeze kwako lazima mwekezaji aje afanye utafiti na kuwaomba wananchi kuendelea kuunga uwekezaji wa bandari na kuwapuuza wanaopinga ambao kimsingi hawalitaki mema taifa.
Naye Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo, alisema kwa kuwa tija ya uwekezaji ina matokeo chanya kwa nchi hivyo serikali ya chama hicho inakaribisha maoni na michango yenye tija ili kuboresha mkataba wa uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.
"Tuko imara tunaruhusu maoni na michango yenye tija ili kuboresha sababu lengo letu ni kutafuta matokeo chanys sio majungu na uzushi usiokuwa na maana," alisema.
Chongolo alisema wanaopinga uwekezaji kimsingi hawana hoja ya msingi na kwamba kwenye dunia ya sasa wananchi watambue kuwa tupo kwenye vita ya ushindani wa kiuchumi na mapambano ya maendeleo ambapo kila taifa halitaki kuona nchi yetu inakuwa kimaendeleo.
"Vita ya uchumi ni vita inayotutaka tukae mguu sawa sababu maeneo au fursa wanazohangaikia ndio hayo hayo ambayo na sisi tunahangaikia,hivyo tusikubali kuyumbushwa kwa maeneo ya uwongo," alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof.Kitila Mkumbo, alisema uwekezaji wa bandari utakuwa na manufaa makubwa sana kwani mapato yatokanayo na bandari yataongezeka kutoka Sh Titrioni 7.7 hadi kufikia Dh.Titrioni 26.7.
Alisema bajeti kuu ya serikali iliyopitishwa na Bunge mwaka huu hivi karibuni ni Sh.Titrioni 44 ambapo kati ya hizo Sh.Titrioni 26 zinakusanywa na serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na zinazobaki serikali inalazimika kukopa au kuongezeka tozo.
"Wataalamu wamebaini tukifanya uwekezaji mzuri wa bandari mapato yataongezeka kutoka Sh.Titrioni 7.7 na kufikia Sh Titrioni 26.7 hivyo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itakuwa na uwezo wa kukusanya Sh Titrioni 52 zaidi ya bajeti ya serikali na hivyo kuondoa mzigo wa kutozwa kodi Watanzania, "alisema.
Pro.Mkumbo alisema uwezo wa bandari ya Dar es Salaam ni kuhudumia mizigo tani milioni 21 kwa mwaka lakini uwekezaji utakapofanyika itakuwa na uwezo wa kuhudumia mizigo tani milioni 50 kwa mwaka.
Kuhusu madai ya mwekezaji kupewa bandari yote, alisema siyo kweli bandari ya Dar es Salaam ina maeneo matatu ambapo eneo la kwanza ni la ndani ambalo lina ukubwa wa hekta 106, eneo la Kurasini hekta 51 na eneo la tatu ambalo lipo Kibaha lina hekta 500.
"Mwekezaji ndani ya bandari ya Dar es Salaam atapewa hekta 7.7 atapewa magati kuanzia 0 hadi 8 na magati mengine watapewa wawekezaji wengine ili washindane na tija itaongezeka na mwekezaji akishindwa kuleta ufanisi ataondolewa na hilo lipo wazi ndani ya mkataba," alisema.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.