Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ali Ussi, ameweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 36 wilayani Mkalama, sambamba na kutembelea programu za Lishe, Malaria na Mazingira.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi hiyo, Ndugu Ussi aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi, na kuwataka wakazi wa wilaya hiyo kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa amani na utulivu.
“Mwaka huu tunauchaguzi Mkuu. Niwaombe wananchi wa Mkalama, itakapofika muda wa kuchagua viongozi wetu, tujitokeze kwa wingi na tushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu. Kupiga kura ni haki yenu ya kidemokrasia,” alisema Ndugu Ussi.
Aidha, aliwasisitiza wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya vyandarua, kula lishe bora na kutunza mazingira ili kuepuka madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
Akizungumza kuhusu miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2025, Ndugu Ussi aliwapongeza viongozi wa wilaya ya Mkalama kwa usimamizi thabiti wa miradi hiyo na kuwataka wananchi kulinda miundombinu ya maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Mwenge wa Uhuru 2025 wilayani Mkalama umeweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo:
•Jiko la Nishati Safi katika Shule ya Sekondari Tumuli,
•Mradi wa maji wa Mbigigi,
•Wodi tatu (wanaume, wanawake na watoto) katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama,
•Barabara ya lami ya Gengerankuru-Moma,
•Mradi wa umwagiliaji wa kilimo Ishinsi,
•Ujenzi wa madarasa sita na matundu kumi ya vyoo, na
•Mradi wa kikundi cha vijana wa bodaboda wa Mkombozi (Kijiji cha Nduguti) ambapo Mwenge ulitoa pikipiki nane kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.