Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka mapema leo aliwaongoza wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuzindua huduma ya bima ya afya iliyoboreshwa.
Bima hiyo sasa itamuwezesha mwananchi mwenye nayo kupata huduma za matibabu kwenye kituo cha Afya au Hospitali yoyote ya serikali na vituo vya afya au hospitali zenye mikataba na serikali ndani au nje ya Wilaya ya Mkalama.
“Unaweza kukuta kuna mtu amekatia bima vyombo vyake vyote vya usafiri na ofisi za biashara lakini yeye mwenyewe na familia yake hawana bima za matibabu, kwa kweli ni lazima tubadilike kwa sababu huwezi kujua ni wakati gani utapatwa na matatizo ya afya” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka pia alibainisha kuwa serikali iliamua kuleta mpango wa bima ya afya iliyoboreshwa ili kupanua wigo mpana zaidi wa huduma za afya kwa wananchi wake hasa baada ya hospitali zote za mikoa kuanza kutoa huduma zinazotolewa na hospitali za rufaa.
“Rai yangu kwa wananchi wote wa wilaya ya Mkalama kila kaya ihakikishe imekata bima hii na bahati nzuri kwa aina hii ya bima kila mwanakaya atapatiwa kadi yake itakayomuwezesha kupata matibabu wakati wowote tofauti na ile ya awali ambayo ilikuwa ikitolewa moja tu kwa kila kaya” Alihitimisha Mhe. Masaka.
Katika hali ya kuonesha kuupokea mpango huo kaya 18 tayari zimeshakata bima hiyo ikiwa ni saa chache tu baada ya kuzinduliwa kwake.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.