Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kupata hati safi kufuatia ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mhe Nchimbi ametoa pongezi hizo muda mfupi uliopita alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano wa baraza la madiwani utakaojikita katika kujadili na kuzipatia ufumbuzi hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mhe. Nchimbi amebainisha kuwa hati hiyo haitokani na viongozi wa Mkoa au Wilaya pekee bali ni matokeo ya ushirikiano baina ya viongozi, watendaji na wananchi wa Wilaya ya Mkalama kwa ujumla.
“Wilaya ya Mkalama ni kama timu ya mpira wa miguu ambapo ili ishinde ni lazima kila mchezaji kwenye nafasi yake atimize wajibu wake na katika hili wananchi pia ni sehemu kubwa sana ya timu hiyo kwa sababu wao si tu wachezaji bali huwa ni washangiliaji pale wanapoona mambo ni mazuri lakini pia huwa ni waamuzi pale wanapoona mambo hayapo sawa ” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amewataka viongozi na watendaji mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama kuitumia ripoti hiyo ya CAG kama kioo cha kuondoa madoa mbalimbali yaliyobainishwa ndani yake ili kwa mwaka ujao wa fedha Halmashauri hiyo iweze kupata hati safi isiyo na madoa.
“Lakini pia nitumie fursa hii kuwapongeza kwa kuwa na ukumbi mzuri na wa kisasa wa mikutano na kwa hili ninaungana nanyi kuwa “Mkalama Nkulu kuliko Iramba” (Mkalama ni kubwa kuliko Iramba). Alimalizia Mhe. Nchimbi.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.