Katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ni muhimu kila mtu kuzingatia kwa dhati elimu na ushauri wanaopata kutoka kwa wataalamu ,Viongozi wa serikali na viongozi wa dini wa kujiepusha na mambo mbalimbali yanayowaingiza katika ushawishi na kuwapelekea kufanya maamuzi yasiyosahihi yanayowapelekea kwenye hatari ya kupata Maabukizi ya UKIMWI.
Hayo yamesema katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo hufanyika Disemba Mosi ya kila mwaka na ambapo kiwilaya ilifanyika katika Kijiji cha Ishinsi Kata ya Msingi.
Akimuwakilisha Mkuu wa wilaya ya Mkalama, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Nduguti Bw. Remigius Ngole amesema kuwa katika kupambana na janga la Ukimwi jamii inatakiwa kujiepusha na vitendo vinavyochochea kujamiana ikiwa ni pamoja na ulevi uliopitiliza pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya .
‘’UKIMWI upo Duniani kote na maambukizi yapo Zaidi kusini mwa Jangwa la Sahara na Tanzania ni moja ya nchi zilizopo eneo hilo .Mkalama sio Kisiwa hivyo mfahamu kwamba UKIMWI upo wilaya ya Mkalama , na hali ya maambukizi ya UKIMWI Kiwilaya kwa kipindi cha January hadi Oktoba ni 2.1% hivyo nawasihi tuendelee kuchukua hatua Madhubuti ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI’’.aliongeza Bw.Ngole.
Awali akisoma risala kwa Mgeni Rasmi Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya wilaya ya Mkalama Bw. Zakaria Lupindo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuendelea kuelimishwa ili kufahamu umuhimu wa kupima afya zao ili wanaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU.
Katika hatua nyingine Bw.Lupindo ameishukuru serikali kuongeza vituo vya Tiba na Mafunzo (CTC) kutoka vituo 5 vivyokuwepo mwanzo hadi 10 kwani imesaidia kusogeza huduma ya tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU ndani ya wilaya ya Mkalama ambapo kwa vituo vyote 10 upatikanaji wa dawa ni 100% ambayo imepunguza usumbufu wa kufuata dawa Nje ya wilaya.
Pia amesema kuwa timu ya uendeshaji afya wilaya hasa waratibu wa UKIMWI wamefanya juhudi za kuhamasisha na kutoa elimu na kuweza kupima wananchi afya zao ambapo kwa kipindi cha January hadi Oktoba jumla ya watu 16,092 ambapo wanaume walikuwa ni 6,324 na wanawake ni 9,770 walipima afya zao na kutambua afya ,walikutwa na na maambukizi ya VVU ni 343 wanaume 136 na wanawake 207 sawa na asilimia 2.1 ya Maambukizi huku walionza huduma ya tiba na mafunzo wakiwa ni 342.
Kila ifikapo tar 1/12ya kila mwaka Tanzania huungana na mataifa yote Duniani kufanya maadhimisho ya siku ya UKIMWI ikiwa na lengo la kutoa elimu ya kujikinga na VVU pamoja na kutathimini hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kupata mapendekezo ya njia bora za kufanya ili kudhibiti maambukizi mapya VVU.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘’ZINGATIA USAWA ,TOKOMEZA UKIMWI ,TOKOMEZA MAGONJWA YA MLIPUKO.’’ikiwa na lengo la kuhimiza usawa katika jitihada zote zinazochukuliwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI na magonjwa mengine ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa homa kali ya mapafu yaani UVIKO 19.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.