Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Dkt. Solomon Michael, ameongoza mafunzo maalum kuhusu magonjwa yasiyopewa kipaumbele, yakiwemo minyoo, kichocho, ngiri na busha, kwa waganga wafawidhi na walimu wa afya. Mafunzo hayo yamefanyika leo Februari 2, 2026, katika ukumbi wa mikutano uliopo Hospitali ya Wilaya ya Mkalama.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Dkt. Solomon amesisitiza umuhimu wa zoezi la chanjo kwa watoto wa shule za msingi, akieleza kuwa chanjo hizo husaidia kuwalinda dhidi ya magonjwa hayo na kuchangia afya njema pamoja na kuongeza ufanisi wao katika masomo.
Aidha, amewatoa hofu wazazi kwa kufafanua kuwa dawa zinazotumika katika zoezi hilo ni salama na hazina madhara. Ameeleza kuwa lengo la zoezi hilo ni kuzuia maambukizi ya minyoo na kichocho kwa watoto, na hivyo amewahimiza wazazi kutowazuia watoto wao kuhudhuria shule siku za zoezi la chanjo, linalotarajiwa kufanyika Jumatano tarehe 4 Februari 2026 na Alhamisi tarehe 5 Februari 2026.
Kwa upande mwingine, Dkt. Solomon amewashukuru walimu kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo na kuwataka kuzingatia kikamilifu maelekezo yote waliyopatiwa, yakiwemo vigezo vya umri wa mtoto anayestahili kupata chanjo—ambapo ni kuanzia miaka mitano—pamoja na kuzingatia urefu wa mtoto kulingana na miongozo ya Wizara ya Afya.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa walimu wa afya kutoka shule zote za msingi pamoja na waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati juu ya utekelezaji bora wa zoezi la chanjo ya minyoo na kichocho kwa watoto wa shule za msingi katika Wilaya ya Mkalama.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.