Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Mfaume Kizigo amepongeza usimamizi wa miradi ya Maji inayoendelea katika kijiji cha Senene kilichopo Kata ya Iguguno na Milade Kata ya Tumuli kwani kukamilika kwa miradi hiyo itapunguza tatizo kubwa la maji kwa Vijiji hivyo.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji Kwa kijiji Cha Senene na Milade Wilayani Mkalama Mkoa wa Singida.
Pamoja na hayo Mhe. Kizigo amefurahishwa na usimamizi wa miradi hiyo kwani ni shirikishi Kwa viongozi wa nyanja zote ikiwepo Vijiji, Kata na Wilaya na kuongeza kuwa hii inaonyesha Wananchi pamoja na viongozi wao wanaunga Mkono juhudi za Serikali ambayo imekua ikitumia fedha nyingi ili kutatua Changamoto za Wananchi kwenye sekta za Elimu, Afya pamoja na maji.
Awali akisoma taarifa Kwa Mkuu wa wilaya ya Mkalama , Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkalama Mhandisi Antidius Muchunguzi amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ya maji itapunguza migogoro kwenye familia inayosababishwa na wakina mama kutumia Muda mwingi kutafuta maji badala ya kuhudumia familia, kupunguza Muda wa upatikanaji wa maji Safi na salama, kupunguza Magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo Safi na salama pamoja na kukuza uchumi kwa wananchi kwa kuwa na Muda mwingi wa uzalishaji Mali.
Aidha, ameongeza kuwa mradi wa Senene unatekelezwa kwa Fedha za Lipa kwa matokeo (P4 R) na umejengwa tanki lenye ukubwa wa Lita 100,000 juu ya ardhi pamoja na fensi wenye thamani ya Tsh. 569,061,004.80 na unatarajiwa kuhudumia wananchi 4,932 na mradi wa Kijiji Cha Milade unatekelezwa kwa Fedha za Mkopo kutoka IMF za Mradi wa 5441 PCRP-UVIKO 19 na unajengwa tanki la Lita 90,000 katika mnara wa mita 9 na fensi wenye thamani ya TSH.502,000,000.00 unatarajia kuhudumia wananchi wapatao 2,088 na miradi yote inatarajiwa kukamili ifikapo mwezi April mwaka 2022.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.