Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba amewataka Watendaji wa Vijiji pamoja na Kata wasiwe chanzo cha migogoro katika maeneo yao na hatimaye kusimama kwa niaba ya Serikali iliyowapa dhamana ya kuongoza kuitatua na kuishughulikia migogoro ikiwepo ya Ardhi.
Ameyasema hayo mapema leo Mei 3, 2023 katika ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi katika Kata ya Nkalakala Kijiji cha Nkalakala Wilayani Mkalama.
Mhe.Serukamba ameliagiza baraza la Ardhi kushughulikia migogoro hiyo pamoja na kuwataka viongozi ndani ya Wilaya ya Mkalama kuwa watetezi wa wanyonge.
‘’nawaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya Vitongoji hadi Wilaya kuhakikisha mnawatetea wanyonge, haiwezekani sisi tupo na wananchi wanendelea kunyanyasika hapana hili jambo halikubaliki kabisa na mimi ni muumini wa kutenda haki’’ Aliongeza Rc Serukamba.
Akizungumzia kuhusu suala la kushuka kwa bei ya Alizeti Mhe. Serukamba aliwataka wakulima kuwa wavumilivu kwani suala hilo linashughulikiwa ikiwa ni pamoja na kuweka kodi kwa mafuta yanayotoka Nchi za nje ili kuhakikisha zao la Alizeti na mafuta yanayozalishwa hapa Nchini yanakuwa na thamani.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwataka Wakulima kujisajili katika Mfumo wa ruzuku ya mbolea itakayowasaidia kuongeza uzalishaji katika mazao yao ambapo amewaahidi wananchi hao kuwa bei ya mbolea ya msimu ujao wa kilimo itakuwa na bei nafuu kuliko msimu uliopita.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.