Muda mfupi uliopita Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahutubia wananchi wa Wilaya ya Mkalama katika Mkutano uliofanyika kwenye moja ya viunga vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Samia ambaye aliambatana katika ziara yake aliambatana na mawaziri watatu, alianza ziara hiyo kwa kukagua miundombinu ya shule ya sekondari Iguguno kabla ya kwenda kuangalia hatua ya ujenzi wa daraja la mto Sibiti na alihitimisha ziara hiyo muda mfupi uliopita kwa kuzindua Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na kuzungumza na wananchi.
Akizungumza kabla ya hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias Kwandikwa alisema kuwa dhamira ya serikali kwa sasa ni kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mkalama hawapati changamoto yoyote kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na ndio maana kwa kushirikiana na Wakala wa barabara wa Taifa (TANROADS) itahakikisha kila upande unaunganishwa kwa kiwango cha lami.
“Hivi karibuni tutaenda kujenga daraja la chuma pale kijiji cha Msingi na wakati wowote fedha ikipatikana kipaumbele chetu kitakuwa ni kuweka lami barabara inayotoka Iguguno hadi daraja la Sibiti huku tukiunganisha pia barabara ya lami kutoka kijiji cha Gumanga hadi Msingi” Alisisitiza Mhe. Kwandikwa.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso alisema kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 10 zimeshatumika kwa miradi ya maji ya Wilaya ya Mkalama ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Kikhonda, Ipuli, Iguguno, Nyahaa na Nduguti ambapo alisisitiza kuwa fedha za miradi hiyo yote zilishalipwa na wananchi wameanza kupata huduma ya maji kwa miradi iliyokamilika.
“Lakini Mhe. Makamu wa Rais ni lazima niseme ukweli kuwa mradi wa maji wa Nyahaa umejaa ufisadi mkubwa sana kwa sababu serikali imelipa zaidi ya shilingi milioni 900 lakini mradi huo haujakamilika mpaka sasa ingawa mkandarasi alishalipwa hela zote na cha kusikitisha zaidi mhandisi aliyekuwa anasimamia mradi huo amehamishiwa Gairo” Alitoa angalizo Mhe. Aweso
Kufuatia hali hiyo Mhe. Aweso alimuomba Makamu wa Rais kumuagiza katibu Mkuu wa Wizara ya Maji amuandikie barua ya wito mhandisi huyo ili afike kwenye kikao cha majumuisho ya Ziara keshokutwa na kutoa majibu ya kina kuhusu suala hilo ombi ambalo Mhe. Makamu wa Rais alilikubali.
Katika hotuba yake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwapongeza viongozi wote wa Wilaya ya Mkalama kwa kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ambapo aliwataka kuendelea kufanya hivyo katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya na miradi mingine ya serikali.
“Lakini lazima niseme ukweli kuwa kitendo cha kusimamishwa pale Ibaga kimeonesha wazi kuwa kuna ukosefu wa ushirikiano baina ya wananchi kwa sababu inaonekana kuna baadhi ya watu wanapangwa kusimama barabarani na mabango kwenye misafara ya viongozi jambo ambalo si zuri na linachafua taswira nzuri mliyoijenga wananchi wa Mkalama” Alisisitiza Mhe. Samia.
Mhe. Samia alihitimisha hotuba yake kwa kuwasihi wananchi wa Mkalama kutunza mazingira hasa katika kipindi hiki cha Masika ili vyanzo vya maji vilivyopo visikauke na kusababisha ukame wakati wa Kiangazi.
“Mwisho ninawaomba Wananchi wa Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla, tujihadhari sana na ugonjwa wa Ukimwi kwa sababu japo sijapata takwimu ya Wilaya lakini takwimu ya Mkoa si nzuri hata kidogo hivyo tujilinde dhidi ya Ugonjwa huu hatari ndugu zangu” Alimalizia Mhe. Samia.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.