Jeshi la zima moto na uokoaji Mkoa wa Singida wametoa mafunzo kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makalama ya namna ya kudhibiti na kujiokoa yanapotokea majanga ya moto wakiwa ofisini hata majumbani.
Mafunzo haya yamefanyika mapema leo Juni 1 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo yalijumuisha Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na watumishi wote wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya.
Akiongea wakati akifungua mafunzo haya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bw. Abdalla Njelu amesema mafunzo haya yatawajengea uwezo watumishi namna ya kutumia vidhibiti moto pindi majanga ya moto yapotokea wakiwa ofisini hata majumbani kwani wengi wao walikuwa hawajui namna ya kutumia vifaa hivyo.
‘’Tumepata taarifa jana kuwa mnakuja kwaajili ya kutoa elimu kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama , kweli leo hii mmekuja kwaajili ya mafunzo naimani elimu hii itawasaidia sana maana najua wengine wanaiona tu ‘fire extinguisher’ lakini hawajui hata kuitumia’’ Aliongeza Bw. Njelu.
Pamoja na hayo Bw. Njelu amewataka kutumia elimu waliyoipata leo kuwa mabalozi kwa wengine pamoja na kutoa msaada wa dharura pale yanapotokea majanga ya moto.
Sajini wa Kituo SSGT. Boniface Wamlamba amesema kuwa jeshi la zima moto na uokoaji linafanya kazi kwa mujibu wa sheria namba 14 ya mwaka 2007 kabla ya kufanyiwa marekebisho ya mwaka 2021 ambayo inafanya shughuli ya kuokoa maisha, kuzima moto pamoja na kusoma ramani za nyumba na kutoa ushauri kabla ya kuanza ujenzi na kutoa huduma kwa jamii.
SSGT. Wamlamba amesema mafunzo wanayotoa yatamsaidia mtu kujua kinga ya tahadhari ya majanga ya moto na vithibiti moto vipi vinapaswa kutumiwa kutokana na aina ya moto kabla ya kutoa taarifa kwenye jeshi la uokoaji na zimamoto kupitia namba yao ya dharura 114.
Akiongea kwaniaba ya watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ,Afisa Maendeleo ya Jamii Bw. Atiki Mohamed amelishukuri Jeshi la Uokoaji na zima moto Mkoa wa Singida kwa mafunzo waliyoyatoa leo ambayo yamewapa dira, elimu na namna ya kufanya inapotokea dharura ya moto ambapo ameahidi watatumia elimu hiyo adhimu kuelimisha jamii namna ya kutumia vithibiti moto hivyo kulingana na madaraja ya moto.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.