“Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye Afya, Timiza wajibu wako” Ni kauli mbiu iliyobeba kampeni ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa Miaka 14 iliyozinduliwa rasmi leo Wilayani Mkalama.
Uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na wananchi, viongozi mbalimbali wa dini na jamii, wanafunzi wa sekondari na wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka.
Katika uzinduzi huo Mhe. Masaka aliwasisitiza wananchi kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 ili wakapate kinga ya saratani hiyo ambayo kila mwaka husababisha vifo vya wanawake 4216 hapa nchini.
“hii ina maana kila siku wastani wa wanawake 11 hufariki dunia hapa nchini kutokana na saratani hii takwimu ambayo ni kubwa sana hivyo wananchi tuhakikishe tunawapa mabinti zetu chanjo hii ili kushusha na kutokomeza kabisa ugonjwa huu kwa akinamama” Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alisisitiza kuwa wananchi wakipata chanjo itawapunguzia gharama za matibabu kwa sababu suala hilo hivi sasa limekuwa mzigo mkubwa sana kwa mwananchi wa kawaida.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. Loth Dia aliwataka wananchi wa Wilaya ya Mkalama kuondoa dhana potofu kuwa chanjo huongeza zaidi maradhi na kuwataka kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea chanjo hiyo.
“Siku za nyuma wanawake wengi walipoteza maisha kwa sababu hakukuwa na chanjo ya Ugonjwa huu hivyo tunaishukuru serikali kwa kuokoa maisha ya kizazi kilichopo kutokana na ugonjwa huu wa saratani ya Mlango wa kizazi na wananchi tuiunge Mkono kwa kuhakikisha watoto wetu wanajitokeza kwa wingi kwenda kupatiwa chanjo hii” Alisema Mhe. Dia.
Kwa mwaka 2018 Wilaya ya Mkalama imelenga kutoa chanjo kwa wasichana 2783 ambao walizaliwa mwaka 2004.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.