Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Daniel Chongolo ameahidi vituo viwili vya Afya Wilayani Mkalama pamoja na kujenga Wodi ya Mama na Mtoto katika kituo cha Afya Kinyangiri ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora katika maeneo yote Wilayani hapa.
Ametoa kauli hiyo Leo March 2 2023 katika ziara yake ya kikazi Wilayani Mkalama yenye lengo la kuimarisha Chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025 kuhakikisha pesa zilizotolewa na Serikali zinafanya maendeleo yaliyokusudiwa na yenye tija kwa Wananchi.
‘’ Nimetembelea kituo cha Afya cha Kinyangiri pamoja na Hospitali ya Wilaya ambayo tayari mmeanza kupata huduma hapo nimeona Kituo cha Afya ni cha miaka ya themanini huko, sasa ninaenda kuongea na Mama nimwambie umenituma Mkalama nimegundua kuna upungufu wa Vituo vya Afya nyie niachieni kazi hiyo kituo kingine kitaenda Iguguno na kingine mtachagua wenyewe ni wapi kipelekwe’’ Aliongeza Chongolo.
Pamoja na hayo amewataka Watumishi wa Afya kuendelea kutoa huduma nzuri kwa Wananchi kutokana na uchache wao huku akisema kuwa Serikali inatambua upungufu wa Watumishi uliopo Nchini na imekuwa ikiajiri kadri ya uwezo ili kuhakikisha wanatatua changamoto za Watumishi ili kuboresha huduma.
Akiongea na wananchi wa Kata ya Iguguno na Nduguti Ndg. Chongolo aliwataka Wazazi kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha Watoto wanapata elimu iliyo bora kwani Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha Sita ambayo imekusudia Taifa kuwa na kizazi cha wasomi watakao shika nafasi mbalimbali hapa Nchini.
Pamoja na hayo Ndg. Chongolo amesema kuwa ataongea na wanaohusika na masuala ya Miundombinu ya Barabara kuhakikisha Wananchi wa Wilaya ya Mkalama wanajengewa Barabara ya kiwango cha Lami kutoka Iguguno kupitia Makao Makuu ya Wilaya Nduguti ambayo itafika hadi Sibiti inayounganisha Mikoa ya Simiyu, Manyara na Arusha.
Awali akitoa taarifa katika Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali alieleza kuwa Wilaya iko salama na Wananchi wanaendelea na shughuli mbalimba za uzalishaji mali na uchumi .
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.