Watoa huduma za Afya Wilayani Mkalama wametakiwa kutoa elimu na kuhamasisha Wazazi na walezi kuhakikisha wanaruhusu Watoto kupatiwa dawa za minyoo tumbo ili kuwakinga na madhara ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos amesema hayo mapema leo Novemba 15. 2022 wakati akifungua mafunzo kwa washiriki takribani 237 watakaotekeleza zoezi la kugawa dawa za kutibu na kukinga maambukizi ya minyoo ya Tumbo, mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheketela Wilayani Mkalama.
‘’Serikali kupitia waaalamu wake hutoa maelekezo ya namna bora ya kuhudumia wananchi wake, hivyo mafunzo haya yakawajengee uwezo wa kufanya zoezi hili kwa umakini mkubwa, na hakikisheni Watoto wote wenye miaka 5 hadi 14 wanakingwa kwa kupatiwa vidonge dhidi ya ugonjwa wa minyoo na tumbo’’ Aliongeza Bi Messos.
Aidha Bi Messos alisema kuwa japo magonjwa hayo yalikuwa hayapewi kipaumbele lakini yamesababisha madhara mengi kwa jamii kama vile maumivu ya muda mrefu , Ulemavu , Umasikini , Ukuaji duni hivyo kuwataka kuwa chachu kwa jamii na kupunguza athari hizo hususani kwa Watoto kushindwa kumudu masomo vizuri.
‘’Nimeambiwa hapa na Mganga Mkuu kuwa pamoja na magonjwa haya hayapewi kipaumbele nimeambiwa hapa kuwa takribani watu Billioni mbili Duniani kote wapo hatarini kupata magonjwa hayo na Nchini Tanzania takribani watu Millioni Tano wameshaambukizwa magonjwa haya’’. Alisisitiza Bi. Messos
Mratibu wa Magonjwa yasiopewa kipaumbele Dr. Julius Nyenje amesema kuwa takribani Watoto 61,247 wenye miaka 5 hadi 14 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Minyoo Wilayani Mkalama hivi karibuni.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.