Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka leo amewaongoza Wananchi wa Wilaya hiyo kwenye maadhimisho ya wiki ya maji yaliyofanyika katika kijiji cha Iguguno.
Maadhimisho hayo yaliambatana na uzinduzi wa visima viwili vya Maji vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 15 vilivyojengwa kwenye kijiji cha Iguguno shamba na Sofia.
Wakati wa uzinduzi huo Mhe. Masaka aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanatumia maji hayo kwa utaratibu mzuri ili waweze kujihakikishia kupata huduma hiyo kwa muda mrefu zaidi.
“Pia naomba mtunze mazingira katika maeneo yote yanayozunguka vyanzo hivi vya maji ikiwemo miti tuliyopanda leo kwa sababu mazingira haya yakiwa mazuri hata uhakika wa upatikanaji wa maji katika maeneo yenu utakuwa ni mkubwa” Aliongeza Mhe. Masaka.
Akisoma hotuba yake ya kuadhimisha kilele cha Wiki ya Maji mbele ya wananchi wa kata ya Iguguno Mhe. Masaka aliipongeza jumuiya ya watumiaji wa Maji pamoja na serikali ya kijiji cha Iguguno kwa kutambua umuhimu wa maji safi kwa jamii inayoizunguka na kuamua kuchimba visima kwenye kijiji cha Iguguno Shamba na Sofia kupitia fedha zao za makusanyo yanayotokana na watumia maji.
“Lakini pia katika miundombinu ya maji iliyopo, vituo vya kuchotea maji pamoja na pampu za mikono vilivyopo ni 736 ambapo vinavyofanya kazi ni 519 huku 217 vikiwa havifanyi kazi hivyo nakuagiza Mhandisi wa maji uhakikishe vituo hivyo vinafanya kazi kabla ya mwezi juni na ikilazimu hata wananchi wenyewe wachangie gharama za utengenezaji wa pampu hizo” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Katika taarifa yake aliyoisoma mbele ya wananchi kwenye maadhimisho hayo, Kaimu Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Antidius Muchunguzi alisema kuwa Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika halmashauri ya Wilaya hiyo kwa sasa imefikia asilimia 61 ikiwa ni sawa na wananchi 129,750 kati ya wananchi 213,674 iikiwa ni ongezeko la asilimia 20 zaidi ya miaka mitatu iliyopita huku akibainisha kuwa kuwa lengo kubwa la idara yake ni kuhakikisha wananchi wote wanaoishi Wilayani hapo wanapata huduma ya maji safi na salama.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka huu yaliambatana na zoezi la upandaji miti 400 kwa vyanzo vya maji vya Nduguti, Kinyangiri, Kikhonda na Iguguno na yalibeba kauli mbiu isemayo “Hakuna atakayeachwa: kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabia nchi”.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.