Mkuu wa Mkoa wa Singida , Mhe. Peter Serukamba ameagiza ofisi ya Mkurugenzi kupitia Idara ya Mifugo kuhakikisha wanawatembelea na kujua maendelea ya hali ya ufugaji kwa kikundi cha Tunza kilichopo Kijiji cha Nduguti Kata ya Nduguti Wilayani Mkalama ili waweze kufuga kisasa na kuweza kujikwamua kiuchumi.
Ametoa maagizo hayo Mei 27 wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya kikundi hicho ambacho kinajishughulisha na ufugaji, Kilimo, kununua mazao mbalimbali pamoja na kulea watoto yatima wapatao watano.
‘’Ninakuagiza Afisa Mifugo wilaya kuwatembelea wanakikundi ili muweze kuwashauri namna ya kufuga kisasa waweze kupata maarifa ya ufugaji bora na wenye tija pia kama walivyoomba wasaidieni kuwapatia elimu ya ujasiriamali’’ Aliongeza Rc Serukamba
Aidha amewapongeza wanakikundi kwa juhudi wanazozifanya kuhakikisha wanatumia fedha vizuri wanazopewa na Serikali kwakujiendeleza na kujikita katika uzalishaji mali pamoja na kurejesha kwa wakati fedha hizo ambapo pia amesema vikundi hivi vinapaswa kufuatiliwa kwa ukaribu ili vifanye vizuri Zaidi kwa maslahi mapana ya wanamkalama.
Katika hatua nyingine Mhe. Serukamba amewataka wanakikundi kuhakikisha wanakata bima ya afya kwaajili ya familia zao ili inapotekea changamoto ya Mwanafamilia ameugua ziweze kuwasaidia kwani suala la afya ni muhimu kwa familia na jamii kwa ujumla.
Awali akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mwenyekiti wa Kikundi cha Tunza Bi. Asha Kiula amesema kikundi kinajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ikiwemo ufagaji , Kilimo pamoja na kununua na kuhifadhi mazao na kuuza pindi bei inapokuwa nzuri ili kujipatia faida na kuongeza mtaji wa kikundi.
Bi Kiula ametaja mafanikio waliyopata kuwa ni pamoja na kupata faida ya kujiinua kiuchumi kwa mwanakikundi mmoja mmoja ambapo wameishukuru serikali kupitia Wizara ya maendeleo ya jamii , jinsia wanawake na makundi maalumu kuendelea kutoa mikopo ya asilimia Nne (4%) kwaajili ya wanawake, na fedha hizo wanakopeshwa na Halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na kwa riba nafuu.
MKALAMA DISTRICT COUNCIL
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.