Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos amewapongeza wananchi wa kijiji cha Mntamba kwa kuchangia fedha katika miradi ya maendeleo na kujitolea nguvu kazi pamoja na mali zao.
Ameyasema hayo leo Novemba 9/2022 wakati akikagua na kutembelea miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi hao kwenye ziara yake ya kikazi inayoendelea Wilayani hapa ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na usimamizi wa matumizi ya fedha za wananchi kwa Vijiji vya Nkinto , Makulo na Mntamba.
Aidha aliwataka wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuendelea kuchochea miradi ya maendeleo pamoja na kuhakikisha wanaweka fedha hizo benki kwa usalama zaidi.
Pia aliwataka wananchi kuendelea kulinda na kuitunza miradi yote inayotekelezwa Wilayani hapa ili idumu kwa vizazi vijavyo.
Katika hatua nyingine alikemea vikali suala la Lambalamba linalotaka kushamiri Wilayani hapa na kusema kuwa yeyote atakayebainika kushirikiana na waganga hao wajadi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwani vitendo hivyo vinachochea migogoro na uvunjifu wa amani katika jamii.
Naye Diwani wa kata ya Nkito Mhe. Reuben Mhai aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kutoa fedha nyingi katika Kata hiyo kwaajili ya ujenzi wa Miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo alisema kuwa watahakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali kwa kusimamia vyema miradi hiyo na kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Katika ziara hiyo aliungana na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kukagua Maendeleo ya ujenzi wa darasa moja shule ya Sekondari Nkinto, mradi wa Shule madarasa mawili (SM2) Sekondari ya Nkinto ,Ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Makulo , Ujenzi wa Zahanati kijiji cha Mntamba ambayo imejengwa kwa nguvu za Wananchi pamoja na Nyumba mbili za walimu kijiji cha Mntamba zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.
Aidha Bi. Asia (Mkurugenzi Mtendaji) alizidi kuupongeza uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mntamba kwa ubunifu wao wa kujenga nyumba ambazo kimsingi zimegharimu kiasi kidogo cha fedha ikilinganishwa na miradi mingine ya iana hiyo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.