MKUU wa Wilaya ya Mkalama , Mhe.Moses Machali, amewataka wananchi kuwa wazalendo na kuuenzi Muungano kwa kufanya kazi kwa bidii.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwakulinda na kutunza miundombinu ya barabara isiharibiwe.
Ameyasema hayo leo April 20, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Kikhonda na Nduguti kijiji cha Mwando kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Machali amesema wananchi wanatakiwa kuonyesha uzalendo na kutii sheria zinazowekwa na mamlaka husika ili kulinda na kutunza miradi mbalimbali ikiwamo ya barabara kwani serikali inatumika fedha nyingi kuigharamia.
"Ninatoa maelekezo kwa yeyote atakayekutwa anaharibu miundombinu ya barabara kwa kupitisha ng’ombe au mkokoteni barabarani faini yake ni shilingi elfu tano kwa kila ng’ombe au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja," alisema Mhe. Machali.
Amesema katika kipindi cha miaka 59 ya muungano, Tanzania inajivunia mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kutatua kero za muungano kwa kuimarisha umoja, mshikamano na usalama uliopo nchini.
Nao baadhi ya wazee waliokuwepo kabla na baada ya uhuru wamesema kuwa wanajivunia muungano kutokana na hapo awali huduma za jamii hazikuwepo Wilayani Mkalama walilazimika kuzifuata Wilaya ya Singida lakini sasa huduma zinawafuata hadi kwenye maeneo yao.
Walisema baadhi ya huduma wanazozipata sasa katika Wilaya ya Mkalama ni pamoja na uwepo wa Shule nyingi za Sekondari na msingi, barabara, umeme na huduma za afya ambazo sasa zinapatikana katika zahanati,vituo vya afya na hospitali ambazo zimejengwa na serikali.
"Maendeleo makubwa yamepatikana ndani ya muungano huu, hivyo tunaahidi kuwaenzi waasisi wa muungano Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume," wamesema wazee hao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.