Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, leo Oktoba 24, 2024, amezindua mradi wa maji na Zahanati yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 436.4 katika wilaya ya Mkalama, mkoani Singida.
Mradi wa maji uliozinduliwa katika kijiji cha Nkalakala, umegharimu shilingi milioni 348.9 na unapunguza changamoto waliyokuwa nayo wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Mkalama, Mhandisi Christopher Saguda, alisema tanki hilo lina uwezo wa lita 90,000 litaweza kuhudumia vituo 12 vya kuchotea maji, huku ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 100.
Mradi mwingine uliozinduliwa na Waziri Silaa ni zahanati ya Igonia iliyopo kijiji cha Mtogo Mwili uliogharimu shilingi Milioni 87.4 ambao ulianza kutekelezwa kwa michango ya wananchi kabla ya Serikali kuendeleza ujenzi wake.
Zahanati hiyo itahudumia vijiji vya Igonia, Ikungu, na Mtamba, ikinufaisha wananchi 1,408 kulingana na sensa ya 2022. Huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za wagonjwa wa nje na uzazi.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Singida,Mhe.Halima Dendego amewatoa hofu wananchi kwa kuwahakikishia upatikanaji wa maji ya kutosha kufikia June 2025 kwa zaidi ya asilimia 100.
"Tunatambua maji ni uhai,na dhamira yetu ya kumtua mama ndoo kichwani ipo pale pale na kweli kinamama ndoo zinashuka kichwani "alisema Mhe.Dendego
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.