Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Singida wameshauriwa kufanya makisio sahihi ya mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa Wakuu wa Idara na Vitengo katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani hatua itakayopelekea ongezeko la mapato na kuondokana na utegemezi kutoka Serikali Kuu.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Menejimenti na ukaguzi Mkoa wa Singida Bw. Evodius Katare Hivi karibuni katika kikao cha kufunga tathimini ya vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri za Mkoa wa Singida jijini Dodoma.
Bw. Katare amesema baadhi ya halmashauri zinakusanya mapato madogo ukilinganisha na hali halisi ya vyanzo vya mapato vilivyopo katika Halmashauri husika na kupelekea upotevu wa mapato ambayo yangetumika kuleta maendeleo.
‘’Inasikitisha sana kuona Idara ndani ya Halmashauri zinakusanya fedha ndogo ukilinganisha na Mshahara ,posho, motisha wanazopewa , unakuta Afisa aliyeaajiriwa kwa kazi inayoleta mapato kwa mwaka mzima anakusanya Mil. 2 hii siyo Afya kabisa kwa Halmashauri’’ Amesema Katare.
Aidha aliongeza kwakuzitaka Idara zinazohusika na ukusanyaji wa Mapato kuwa makini na kujitoa kwaajili ya kazi hizi na kuwataka kufanya kazi kwa Moyo kuhakikisha hakuna upotevu wa mapato na kuacha uvivu unaopelekea kutojali ukusanyaji wa fedha za Serikali.
Bw. Rwakatare amewashauri Wakurugenzi kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa Halmashauri zilizofanya vizuri katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani ili kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuona namna bora ya kuongeza mapato katika Halmashauri husika.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Mkoa wa Singida Bi. Nteghenjwa Hosseah amesema kuwa ofisi ya TAMISEMI katika zoezi hili imegundua kuna baadhi ya ushuru wanakusanya Halmashauri moja huku zingine zikiwa hazikusanyi, ambapo alisema ufika wakati Mkoa uweke utaratibu wa Halmashauri zote kukusanya kwenye vyanzo vinavyofanana bila kuwa na utofauti.
Zoezi hili limetoa fursa kwa Wataalamu wa Halmshauri za Mkoa wa Singida kupitia bajeti zao kwa kina , kuongeza wigo wa mapato , kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuandaa bajeti yenye uhalisia.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.