Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Mfaume Kizigo amewataka wakulima kujiandaa mapema na msimu wa kilimo kwa kufuata njia bora za kilimo ili kuwa na chakula cha kutosha na kukuza uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo jana katika ziara yake ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kijiji cha Ishinsi Kata ya Msingi Wilaya ya Mkalama.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya Kizigo aliwataka wananchi kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kusajili wakulima wote kwenye mfumo ili waweze kupata ruzuku ya mbolea kwa bei nafuu.
‘’ninawashauri wakulima kujisajili ili mpate ruzuku ya mbolea, Serikali imesikia kilio chenu kutokana na bei ya mbolea kuwa juu sana , kuna faida kubwa sana za kukopeshwa mbegu na Serikali’’.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuibua miradi ili Serikali inapotoa fedha iwe rahisi kupeleka sehemu ambayo tayari kuna kitu kinaendelea .
‘’Ninaomba wananchi muwe tayari kuanzisha maboma ili inapotokea tumepata fungu Serikalini iwe rahisi kupeleka sehemu yenye mradi tayari, anayepewa lifti ni yule aliyepo barabarani’’ Aliongeza Dc Kizigo.
Hata hivyo, alisema kuwa serikali ya awamu ya Sita imelenga kutatua kero za Wananchi katika masuala ya Afya , Elimu ,Kilimo , Maji , Umeme na huduma hizo kumfikia Mwananchi popote alipo kwa ustawi wa jamii.
Afisa kilimo , Mifugo na uvuvi Wilaya ya Mkalama Selemani Msunga alisema kuwa Serikali imekusudia kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na sasa imeanza kuandikisha wakulima katika mfumo ili wapate ruzuku ya mbolea na kusema hadi sasa Takribani Wakulima 7200 wameonekana kwenye mfumo na zoezi linaendelea huku akiwataka wakulima kuendelea kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo.
Aidha, Bw. Msunga aliongeza kuwa Alizeti itabaki kuwa zao la kimkakati wilaya ya Mkalama licha ya changamoto zilizojitokeza Msimu wa Kilimo wa mwaka jana ambapo Serikali ilitoa mbegu ambazo hazikuwa na mavuno mazuri kwa wakulima na kuongeza kuwa kwa msimu wa mwaka huu 2022 Serikali itaendelea kutoa mbegu zilizo bora ili kuhakikisha zao la Alizeti linalimwa kwa wingi.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Msingi walimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika kwenye maeneo yao ili kusikiliza kero zao na kutatua changamoto walizonazo wamesema wanaimani na serikali ya awamu ya Sita kuwa watawapelekea huduma nyingi za maendeleo ikiwepo umeme kufika kila kitongoji ili wananchi waweze kukua kiuchumi na kukuza pato lao binafsi na Halmashauri.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.