Wajumbe wa Halmashauri ya Serikali ya vijiji vya Munguli, Ikolo na Endasiku wametakiwa kusimamia miradi yote inayotolewa na Serikali kwa niaba ya Wananchi na kuitambulisha kwao ili kuwajengea ufahamu wa nini kinaendelea katika maeneo yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos ameyasema hayo leo tar 8/11 /2022 katika ziara yake ya kikazi kwa Vijiji vya Munguli, Ikolo na Endasiku Kata ya Mwangeza wilayani Mkalama.
Aidha alieleza lengo la ziara yake kuwa ni kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani hapa pamoja na kujiridhisha fedha zinazochangwa na wananchi zimefanya shughuli iliyokusidiwa pamoja na gharama za miradi kama zinaendana na fedha halisi.
Pamoja na hayo aliwataka Wajumbe wa Halmashauri ya Serikali ya vijiji kusimamia ukusanyaji wa mapato pamoja na kuandaa taarifa ya mapato na matumizi ili kuweka wazi kwa wananchi kwani wao ndio wamekuwa wachangiaji wa fedha za maendeleo katika maeneo yao.
‘’Ninakuagiza Mtendaji wa Kata kuwasimamia watendaji wa Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vijiji kuandaa taarifa ya mchanganuo wa makusanyo yote ya michango ya Wananchi na ninawaagiza kuhakikisha mnafanya vikao vya kisheria kwani huko ndiko mtatoa taarifa za mapato na matumizi yatokanayo na michango yaO’’ Aliongeza DED Messos.
Hata hivyo alimuagiza mtendaji wa Kata kuhakikisha ndani ya miezi mitatu wanakamilisha Mradi wa ujenzi wa Madarasa mawili ujulikanayo kama Shule Madarasa Mawili (SM2) ili kuhakikisha changamoto ya madarasa inatatuliwa wilayani hapa na wanafunzi wasome bila usumbufu wa kukosa madarasa.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wilayani Mkalama Bi Lilian Kasanga alitumia kikao hicho kuwataka wanaosimamia miradi ya ujenzi kuhakikisha wanakuwa na mikataba baina yao na Wakandarasi ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza kabla ya kukamilisha kazi pamoja na kuunda kamati ya ujenzi na Manunuzi ili kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi vinanunuliwa na kusimamiwa na kamati husika.
Ziara hiyo ni Endelevu na kesho tar 9/11 2022 itafanyika Kata ya Nkinto.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.