Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge amewataka wajumbe wa baraza la Ardhi na nyumba wilaya ya Mkalama kutumia hekima na busara katika kutatua kesi zinazohusu migogoro ya Ardhi wilayani hapa Ili haki iweze kutendeka kwa wote.
Ameyasema hayo mapema leo wakati akiwaapisha wajumbe wa baraza la Ardhi na nyumba wilayani hapa katika ukumbi wa Sheketela uliopo halmashauri ya wilaya ya Mkalama Mkoani Singida.
Dkt Mahenge amewataka wajumbe hao kusoma nyaraka zote na kupitia mashauri yaliyotatuliwa na baraza lililopita ili kujifunza na sio kuanza kutatua kesi kabla ya kujifunza na kuamua kwa matakwa yao .
" Mnakwenda kutatua kero za wananchi na kero zilizo nyingi kwa wananchi Kimkoa , kiwilaya na Kata ni migogoro ya ardhi hivyo mkatumie hekima busara katika kutenda haki na msio chanzo cha migogoro" Aliongeza Dkt Mahenge Rc Mkoa wa Singida.
Pamoja na hayo aliwapongeza wajumbe hao kwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa baraza hilo na kuwa miongoni mwa wachache waliopata nafasi hiyo kati ya wengi walioomba nafasi na kuwataka kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana na mwenyekiti wa baraza la Ardhi wilaya katika kutumikia wananchi.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo aliwataka wajumbe hao kuwa kiungo Cha kuunganisha familia zilizofarakana kutokana na migogoro ya ardhi Kwa kutenda haki kwa uadilifu Mkubwa huku akiwataka kutumia nafasi zao vizuri na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama Mhe.James Mkwega amesema kuwa tukio hilo ni la kihistoria kwani toka kauanzishwa Kwa wilaya mwaka 2014 hakujawahi kuwa na baraza la Ardhi kitu kilichopelekea wananchi kukosa haki kwa kushindwa kufuata huduma wilayani Iramba kutokana na umbali uliopo kutoka Mkalama hadi Iramba hivyo kuwataka wajumbe kutenda haki kwa kuzingatia taratibu na viapo vyao.
Mwenyekiti wa baraza la Ardhi na nyumba wilaya ya Mkalama na Iramba Baraka shuma amesema kuwa baada ya mchakato kufanyika kuwapata wajumbe hao kilichofuata ni kula kiapo kwaajili ya kuanza majukumu yao huku akipongeza kupatikana kwao kwani itapelekea kurahisisha upatikanaji wa huduma wilayani Mkalama kwani wananchi wengi walipoteza haki zao kwakushindwa kufika wilayani Iramba kutokana na umbali na sababu zingine ikiwemo umri na kipato kidogo hivyo kupelekea haki zao kupotea.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos alieza mchakato wa maandalizi wa zoezi la kukusanya taarifa za Anuani za Makazi na Postikodi katika Wilaya ya Mkalama kuwa unaendelea vizuri na hadi kufikia Sasa tayari wameshapata majina ya vijana wazalendo 350 watakao fanya kazi hiyo ambapo walitumia watendaji wa kata kuwapata vijana hao waadilifu na wazalendo huku vijana waliohitimu mafunzo ya jeshi la akiba wakipewa kipaumbele.
Sanjari na hayo amesema kuwa tayari elimu imetolewa Kwa wajumbe wa sensa ngazi ya kijiji na kitongoji ambapo watendaji wa kata walitakiwa kutambua makadirio ya Anuani za Makazi na tayari zoezi hilo limefanikiwa nakubaini Anuani za Makazi elfu arobaini na Tano (45,000) na wiki ijayo hamasa itaanza kutolewa kwa wananchi ya namna ya kushiriki katika zoezi la kukusanya taarifa za Anuani za Makazi na Postikodi pamoja na sensa ya watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti Mwaka huu.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.