Wafugaji wilayani Mkalama wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchanja mifugo yao, kwani ufugaji wenye tija ni ule unaolenga kuongeza ubora wa mazao yatokanayo na mifugo na kumnufaisha mfugaji katika kukuza pato la familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema hayo mapema leo wakati akizindua zoezi la chanjo ya Mifugo dhidi ya ugonjwa wa Kimeta ,Chambavu kwa Ng’ombe na na Minyoo na homa ya mapafu kwa mbuzi na Kondoo katika kijiji cha Kinampundu , Kata ya Kinampundu wilayani Mkalama.
‘’Niwasihi wafugaji kuhakikisha mnaleta mifugo yenu yote ili ipatiwe chanjo ili kuikinga na ugonjwa wa kimeta, na mtaalamu katuambia hapa kuwa ugonjwa huu ni tishio kwa mifugo yetu na kwa bindamu tusipuuze zoezi hili kwani wataalamu wamekuja kwenye maeneo yetu imebaki nyie tu kuleta mifugo hapa ili ichanjwe kuepuka madhara hayo’’. Aliongeza Dc Kizigo.
Pamoja na hayo ameagiza ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kuona namna ya kutafuta mbegu za majani ya malisho na kugawa kwa wafugaji , ili wapande kwenye maeneo ya malisho kwani kwakufanya hivyo itapelekea mifugo kupata majani ya kutosha na kuwa na afya bora hivyo kuongeza upatikanaji wa soko la mifugo na kukuza pato la wilaya.
Awali akisoma Risala kwa Mgeni Rasmi Afisa Mifugo wilaya ya Mkalama Elias Mbwambo alisema kuwa zoezi hilo ni kutekeleza sera ya chama cha mapinduzi na takwa la kisheria ambapo sheria ya udhibiti wa magonjwa namba 17 ya mwaka 2003 inaagiza mifugo yote ipatiwe chanjo ili kuzuia vifo vya mifugo na ueneaji wa magonjwa ya Mlipuko kwa wanyama na binadamu, na usimamizi wa sera ya mwaka 2006 inayosisitiza ufugaji wa kibiashara wenye tija na ushindani wa kimataifa katika uvuvi na ufugaji ili kuunga mkono wafugaji wadogo waweze kuwa wajasiliamali wazuri.
Aidha Mbwambo aliongeza kuwa zoez hili ni endelevu katika wilaya ya Mkalama toka mwaka 2003 ambapo limekua likifanyika kila mwaka na limeleta mafanikio makubwa kwani vifo vitokanavyo na magonjwa ya mifugo vimepungua kutoka asilimia 22 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 4 mwaka 2021 huku akitaja changamoto kwa baadhi ya wafugaji kupuuza juhudi za serikali za kupambana na magonjwa ya mlipuko kwa mifugo yao na kuficha mifugo isipate chanjo hivyo kupelekea hasara ndani ya familia na kwa wilaya pia.
Pamoja na hayo alisema kuwa wilaya imejipanga kuchanja Ng’ombe 90,727 Mbuzi 79,158 , Kondoo 40,271 na zoezi hili litachukua takribani siku kumi na Nne na watapita kwenye Vitongoji vyote na Vijiji vyote vya Wilaya ya Mkalama.
Diwani wa Kata ya Kinampundu Silvester Marimo alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa mpango wake kabambe wa kupambana na magonjwa yanayoikabili mifugo ambapo pia alisema watatumia fursa hiyo kuwahamasisha wafugaji kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo huku akiiomba Serikali kuwajengea vibanio vya kudumu kwaajili ya kuingiza Ng’ombe wanapochanjwa kwani wanavyotumia sasa ni va kienyeji na sio vya kudumu.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.