Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka amewataka wafugaji waliopo Wilayani hapa kuhakikisha wanalisha mifugo yao katika maeneo waliyotengewa badala ya kuipeleka katika kila eneo la wazi wanaloliona.
Mhe: Masaka ameyasema hayo wakati akizindua zoezi la upigaji chapa Mifugo Wilayani Mkalama ambapo aliwashauri wafugaji hao kujiunga na vyama vya ushirika ili kufanya shughuli zao kwa faida tofauti na sasa ambapo kila mfugaji anafanya shughuli zake mwenyewe hali inayosababisha kutotengeneza faida kubwa.
“ Lakini pia baada ya kujiunga kwenye vyama hivyo tumieni sehemu ya faida mnayopata kuchangia shughuli za maendeleo kwa sababu maendeleo ya Wilaya hii yanaletwa na sisi sote kwa pamoja” Ameongeza Masaka.
Katika hatua nyingine Mhe: Masaka amewataka wafugaji hao kuhakikisha wanafuata taratibu za ufugaji wa kisasa ili mifugo yao iwe na afya kwa ajili ya kuanza kusafirisha nje ya Nchi.
“ Inawezekana nyama inayosifiwa na kuliwa nje ya nchi ikawa inatokana na Ng’ombe waliopo Tanzania hivyo ni vyema kuweka mifumo ambayo itatusaidia kupata faida pindi tukiuza mifugo yetu nje ya nchi” Amesema Masaka.
Amesema kuwa hatua ya kuuza mifugo hiyo kimataifa huwa inaanza pale Ng’ombe wanapouzwa katika soko la Mkoa wa Singida na hatimaye kusafirishwa mpaka nje ya Mkoa huo ambapo huko hukusanywa kabla ya kusafirishwa mpaka nje ya nchi.
Akizungumza mapema kabla ya kumkaribisha Mhe: Mkuu wa Wilaya, Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Mkalama bw. Elias Mbwambo amesema kuwa pamoja na kuanza na tarafa ya Kinyangiri kwa mujibu wa ratiba, Zoezi hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
“Katika zoezi hili mfugaji atalazimika kulipia shilingi mia tano kwa kila ng’ombe atakayepigwa chapa ili gharama hizo zitumike kufanikisha zoezi hili katika maeneo mengine tunayoendelea nayo na ng’ombe watakaohusika na zoezi hili ni kuanzia ndama wa miezi sita na kuendelea” Amesema Mbwambo.
Mbwambo amesema kuwa zoezi hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa sana udhibiti wizi wa mifugo kwani sasa mifugo itakuwa na alama inayoonesha ilipotoka na pia itasaidia katika harakati za udhibiti wa magonjwa ya mifugo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.