Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amewataka viongozi wa dini wilayani hapa kutumia vyema nafasi zao kuelemisha wananchi kuhusu kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuhubiri maadili mema nchini.
Wito huo ameutoa Septemba 20,2024 wakati wa kikao na viongozi wa dini mbalimbali wilayani hapa kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu mmonyoko wa maadili, suala la uzalendo, amani pamoja na ushiriki wa viongozi hao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
“Ningependa kutumia nafasi hii kuwataka mkawajuze waumini kuhusu kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakofanyika tarehe 27.11.2024 kwa amani na upendo. Tujitokeze kwa wingi katika kampeni, tujiandikishe kwenye daftari la Orodha ya wapiga Kura kuanzia Oktoba 11-20, 2024 lakini pia siku ya uchaguzi tuchague viongizi wetu kwa amani” Mhe. Machali
Vile vile Mhe. Moses Machali amewakumbusha viongozi hao wa dini kuhusu zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutumia nafasi zao kuwaeleza wananchi ifikapo Septemba 25,2024 wajitokeze kuboresha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2025 “Uboreshaji utafanyika kwa siku saba kuanzia Septemba 25- Oktoba 1,2024, hivyo tujikoze kwa wingi pia” Mhe. Machali
Akizungumzia kuhusu suala la maadili pamoja na amani nchini, Mh. Moses Machali amesema viongozi wa dini wanajukumu kubwa katika kuhubiri amani pamoja na kulinda maadili ya jamii za kitanzania,“Twendeni tukahubiri amani na upendo kwa waumini wetu, nitashangaa siku nikisikia watu wa Mkalama wanagombana kwasababu ya dini, kila mmoja aheshimu imani ya mwenzake” Mhe. Machali
Kwa upande wake Mchungaji Manase Msengi, kutoka kanisa la KKT Ushirika wa Nduguti, ambaye amezungumza kwa niaba ya viongozi hao, amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa wilaya ya Mkalama kwa kukutana na viongozi wa dini kwa ajili ya kujadili masuala ya maadili, uzalendo na amani hasa katika kipindi hiki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wananchi wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.