*Hakuna gharama usajili wa wakulima mfumo wa mbolea za ruzuku*
#wakulima watakiwa kujisajili kabla ya msimu wa kilimo kuanza
Imeelezwa kuwa usajili wa wakulima kwa ajili ya kunufaika na mbolea za ruzuku hauna gharama yeyote na yeyoye atakayewatoza kiasi chochote cha pesa wakulima atachumuliwa hatua.
Hayo yamesemwa Oktoba 5 2022 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa hafla ya kuzindua msimu wa kilimo kwa mwaka 2022/2023 uliofanyika katika ukumbi wa kanisa katoliki mkoani Singida.
Waziri Bashe ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo kwa kusimamia na kuhakikisha Mfumo wa kielekitroniki wa mbolea za ruzuku unapatikana.
"Amesema awali jambo la kuwa na mfumo wa kuuza mbolea ya ruzuku lilionekana kuwa ni gumu lakini Dkt. Ngailo amelisimamia nankulifanya kuwa halisi" waziri Bashe aliongeza.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Ngailo ametoa rai kwa wakulima wote nchini kujisajili kwenye ofisi za vijiji na vitongoji wanakofanyia shughuli za kilimo ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa msimu wa kilimo 2022 /2023.
Amesema, serikali imetoa ruzuku za mbolea kwa msimu huu wa kilimo ili kunufaika na ruzuku ya mbolea ni lazima mkulima ajisajili na kueleza kuwa sharti kubwa la mkulima kusajiliwa ni kuwa na shamba, vinginevyo hakuna masharti mengine.
Aidha, Dkt. Ngailo amewataka wakulima kutoa taarifa sahihi juu ya ukubwa wa mashamba wanayoyalima ili kusaidia katika kununua mbolea itakayokidhi mahitaji kwani ukubwa wa shamba ndio utaamua ni kiasi gani cha mbolea unapaswa kununua.
Amesema, kwa sasa Serikali inawaandikisha wakulima kwa kuchukua taarifa zao za msingi ili waweze kupata huduma ya mbolea kwa wakati na kubainisha kuwa hapo baadaye wakulima watapigwa picha pamoja na kuchukuliwa alama za vidole ili kupunguza ubadhirifu unaofanywa na watu wasiokuwa waaminifu na hivyo kuwanufaisha wakulima hewa kwa mbolea za ruzuku.
Pia, Dkt. Ngailo alisema baada ya usajili huo wa awali, Serikali imedhamiria kupita kwa kutumia GPS katika maeneo waliyojiandikisha wakulima ili kuhakiki ukubwa wa mashamba yaliyojazwa wakati wa usajili na hivyo kuwataka wakulima kutoa taarifa sahihi za maeneo wanayolima.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.