Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amesema kuwa hali ya usalama wa Maisha ya Watoto wilayani Mkalama sio shwari kutokana na Watoto kukumbwa na vifo vitokanavyo na kutumbukia kwenye madimbwi na mashimo ya choo ambayo hayajafunikwa .
Mhe. Machali amesema hayo leo Februari 20, 2023 kwenye kikao kazi cha Waratibu wa Elimu Kata, Walimu wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi, Watendaji wa Kata na Vijiji , Maafisa maendeleo ya jamii Pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama.
‘’Mashimo yanachimbwa yanaachwa wazi maji yanajaa na hii mvua inavyonyesha hivi majuzi kumetokea vifo vya namna hii, nilivyofanya uchunguzi wangu nikasikia wananchi wanasema wakifa watu wawili afadhali maana tumezoea kufa hata zaidi ya Watu ishirini nilishangaa sana’’ Alisema Mhe. Machali
Aidha Mhe. Machali aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanalinda haki za Watoto na raia ikiwepo haki ya kuishi, kwa kuwataka watendaji wa Kijiji wakishirikiana na Watendaji wa Kata kutekeleza jukumu hilo kupitia elimu kwa wananchi waochimba mashimo kuhakikisha yanafunikwa ili kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
‘’kwa tafsiri hii baada ya kutoa maelekezo haya nitakaposikia kuna kifo chochote kinatokana na Shimo wewe Mtendaji nitaaza na wewe ninawapa kipindi cha wiki moja nendeni mkashughulikie suala hili sitaki kusikia vifo vinavyotokana na uzembe’’ Alisisitiza Mhe. Machali
Pamoja na hayo amewataka watendaji hao kuongeza juhudi na kasi kwenye kuhakikisha ulinzi wa mali na Raia kwani serikali iliwaamini na kuwapa nafasi hizo za uongozi.
Hata hivyo amewataka Watendaji hao kuwachukulia hatua kali za kisheria wananchi watakao kiuka maelekezo yote aliyoyatoa leo .
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.