Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama pamoja na Kanisa la Maranasa Kata ya Nduguti leo wametoa msaada wa chakula na mavazi kwa wakoma 140 waishio katika Kijiji cha Nkungi ili waweze kusherehekea vema sikukuu za Mwisho wa mwaka huu.
Akikabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo alisema kuwa msaada huo umelenga kuhakikisha wakoma hao wanasherehekea sikukuu kwa furaha ambapo amewatia moyo kwa kuwataka kutokata tamaa kutokana na changamoto waliyonayo na kuwatia moyo kwani matatizo waliyonayo kwani inaweza kumpata yeyote.
‘’Leo tumekuja kuongea na nyie na kufurahi na nyie katika kipindi hiki cha kuelekea Mwisho wa mwaka najua mna changamoto nyingi lakini leo tumekuja kufurahi na sio kusikiliza changamoto’’. Amesema Mhe. Kizigo
Mhe. Kizigo amebainisha kuwa wapo watu wenye ulemavu unaoonekana na usioonekana hivyo jamii inapaswa kuishi na watu hao kwa usawa na kutowanyanyapaa kwa namna yoyote.
"Nimedokezwa na Mwenyekiti wenu hapa kuwa mmetoka kujishugulisha hivyo niwapongeze sana kwani pamoja na hali mliyonayo bado mnajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia maendeleo ya Wilaya ya Mkalama na Taifa kwa ujumla" Ameongeza Mhe. Kizigo.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa msaada uliotolewa leo Bi Helena Samweli na Bw. Ilanda Salehe wameushukuru uongozi wa Wilaya ya Mkalama kwa kuwapelekea msaada huo na kuwasisitiza wasisite kufanya hivyo wanapopata nafasi kwani kitendo hicho kimewafanya wajisikie wenye furaha na kuthaminiwa na Viongozi wa ngazi za juu.
Uongozi wa Wilaya ya Mkalama kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali umekuwa na utamaduni wa kuwatembelea na kupeleka misaada kwa jamii hiyo ambayo imekuwa ikiishi na changamoto ya kuathiriwa na Ugonjwa wa Ukoma kwa muda mrefu ambapo Msaada uliotolewa leo ni pamoja na Mahindi, Mchele, Sabuni, Sukari pamoja na nguo na Mashuka ya kujifunika.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.