Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka jana alitoa msaada wa chakula na mavazi kwa wahanga wa ugonjwa wa ukoma maarufu kama ‘wakoma’ wanaoishi katika kijiji cha Iambi Wilayani Mkalama.
Msaada huo umetokana na jitihada za dhati za Mhe. Masaka za kutafuta wadau mbalimbali wa kuwasaidia wahanga hao na unajumuisha magunia 18 ya mahindi na viroba vitatu vya nguo ambazo hazijachakaa.
“Shukrani zangu za dhati ziende kwa kanisa la EAGT, kanisa la Maranatha,kanisa la KKKT wanzelya lililopo hapa Nkungi na watu binafsi ambao wametoa na wanaendelea kutoa michango mbalimbali kwa ajili ya wahanga hawa” Alisema Mhe. Masaka.
Naye Mwenyekiti wa shirika lisilo la serikali linalowasimamia wahanga hao (CHADEREREKO) bw. Martin Nakomolwa amemshukuru Mhe. Masaka kwa jitihada zake za dhati za kuwasaidia wahanga hao na kuongeza kuwa hakuna Mkuu wa Wilaya ambaye amewahi kusimamia kikamilifu jambo hilo zaidi yake.
“Wote hapa ni mashahidi kuwa wamepita wengi katika Wilaya hii lakini hakuna aliyewahi kuguswa na suala la wakoma kwa kweli Mungu aendelee kukudumisha katika Wilaya yetu” Aliongeza Nakomolwa.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Diwani wa kata ya Ilunda Mhe. Mohamedi Imbele amesema kuwa ni vyema misaada hiyo ikatumiwa na walengwa ili kuweza kutimiza haja ya wote waliojitolea kuwasaidia wahanga hao.
“Lakini mimi pia ntakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wilaya yetu hasa kupigania haki za wanyonge jambo ambalo ndio hasa muelekeo wa serikali ya awamu hii” Alimalizia Mhe. Imbele.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka alitumia nafasi hiyo kugawa vifaa mbalimbali kwa watu wawili wenye albinism ambapo jumla ya kofia za kujikinga na jua nne, Mafuta maalum ya ngozi, miwani pea nne iligawiwa kwa watu hao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.