Umoja wa Wakazi wenye asili ya Wilaya ya Iramba na Mkalama (IDA) umetoa msaada wa jezi pea mbili kwa timu ya Wilaya ya Mkalama inayotarajia kushiriki mashindano ya Umitashumta katika ngazi ya Mkoa.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka ambaye pia ndo alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi, aliwashukuru wajumbe wa umoja huo kwa uzalendo waliouonesha kwa timu hiyo na kuongeza kuwa si rahisi kwa watu walioondoka katika maeneo yao ya asili kukumbuka kupeleka misaada katika maeneo yao.
“Binafsi kwa kuteuliwa tu kuwa Mkuu wa Wilaya tayari nimeshakuwa mwanachama wa Umoja huu ndio maana nahakikisha Wilaya ya Mkalama inasonga mbele katika Nyanja zote” Alisema Masaka.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga ametoa rai kwa watu wengine kuiga mfano uliooneshwa na Umoja huo na kuongeza kuwa wamefanya jambo la kizalendo sana na linalopaswa kuenziwa.
“ Tunaomba msiishie hapa tu bali tuendelee kushirikiana katika kutatua kero mbalimbali za wananchi wa Mkalama” Aliongeza Sanga.
Naye Mwenyekiti wa Umoja huo Bw. Joseph Nsoza alisema kuwa amefarijika sana kwa jinsi Wilaya ya Mkalama ilivyopiga hatua hali ambayo ni tofauti kabisa na kipindi walipokuwa wanaondoka na kuupongeza uongozi wote wa Wilaya kwa kazi ngumu ya kuhakikisha Mkalama inazidi kuwa bora kila siku.
“ Wakati tunaondoka hapa nyumbani palikuwa nyuma sana kimaendeleo lakini leo hii tumekuja na kuikuta Mkalama yetu mpya kabisa na inayozidi kuendelea, tumefarijika sana kwa hili” Alisema Nsoza.
Nsoza alimaliza kwa kuahidi kuutumia umoja huo kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Wilaya hiyo na kwamba malengo ya Umoja huo na ya Wilaya yanalingana.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.