Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali leo Machi 11,2024 amefanya ziara ya kikazi katika Kijiji Cha Mdilika na Singa Kata ya Kinampundu kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa vijiji hivyo.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Singa na Mdilika, Mhe. Moses Machali amewaambia wananchi kuwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inaenda kuwa historia kwani serikali tayari imeweka mpango wa kupeleka maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Chini ya Rais Samia serikali imenunua magari na kuyasambaza mikoa yote Tanzania Bara, na mkoa wa Singida tumepokea gari hilo jipya. Gari hilo linafanya kazi ya kuchimba visima vijijini na mijini. Hivyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 kufikia mwezi wa 12 naamini RUWASA watakuwa wamefanya jambo hapa”. Mh.Moses Machali.
Mbali na hilo Mkuu wa wilaya Mhe. Moses Machali amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutunza miundombinu ya miradi inayotekelezwa na serikali ili kuipa nguvu serikali kwa kuwaletea maendeleo mbalimbali.
Awali akijibu maswali kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama, Meneja wa RUWASA wilaya ya Mkalama. Mhandisi Christopher Saguda amesema jumla ya Tsh 362,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kusambaza maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vya Singa na Mdilika.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga Tsh 212,000,000 kwa ajili ya kusambaza maji katika Kijiji cha Mdilika na pia serikali itapeleka Tsh 150,000,000 kwa ajili ya kusambaza maji safi na salama katika Kijiji cha Singa” Mhandisi Saguda.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.