Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni chombo kilichosaidia kwa kiasi kikubwa sana kukuza na kuboresha kiwango cha Elimu nchini kwa kuwezesha miundombinu inayozunguka sekta hiyo nyeti kabisa Ulimwenguni hivi sasa.
Katika Wilaya ya Mkalama, Mamlaka hiyo imewezesha kupatikana kwa miradi mikubwa miwili ambayo kwa namna moja au nyingine itasaidia kuinua kiwango cha udahili na ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Kitongoji cha Munguli ni eneo linapoishi kabila maarufu sana la Wahdzabe ambalo kwa miaka mingi tangu kupatikana kwa Uhuru limekuwa na mwitikio mdogo linapokuja suala la elimu hasa kutokana na kabila hilo kuishi mbali sana na mahali zinapopatikana huduma za kijamii.
Baada ya kuona changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kushirikiana na TEA wameanza Ujenzi wa bweni na bwalo la chakula la kisasa kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Munguli mradi ambao ukikamilika utaongeza hamasa kwa jamii hiyo kushiriki katika haki yao ya Msingi ya kupata Elimu kwa kusaidia wanafunzi hao kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu mpaka kufika shuleni na pia itawahakikishia kupata huduma bora ya chakula kwa wakati hali itakayowawezesha kupata muda mrefu zaidi wa kukaa shuleni.
Kwa mujibu wa Mkadiriaji wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Paskazia Tibalinda Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 184 kwa upande wa bweni na shilingi milioni 119 kwa upande wa bwalo na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.
“Zoezi la uchimbaji wa msingi limechukua muda mrefu kidogo kutokana na uwepo wa mawe kwenye udongo wa eneo hili lakini tunashukuru tumemaliza na sasa kinachofuatia na kumwaga kifusi na jamvi ambapo baada ya hapo kazi hii itaanza kwenda kwa kasi” Aliongeza Bi. Tibalinda.
Akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Elimu Tanzania wakati wa ziara ya ukaguzi wa mrad huo, Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi. Sylvia Lupembe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa usimamizi mzuri wa mradi huo ambapo ametoa rai ya kukamilika kwa mradi huo kwa wakati na katika ubora ulioanza nao.
“Mradi huu ni maalum kwa sababu utaisaidia jamii maalum ya Watanzania kabila la wahadzabe lakini pia utaibadilisha jamii hii kama ambavyo wenyewe wamesema kuwa wamekaa sana porini lakini hawatoacha Mila yao ila wanahitaji kupata elimu” Aliongeza Bi. Lupembe.
Bi. Lupembe ameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa chachu ya kuchochea maendeleo ya Elimu kwa kuongeza idadi ya udahili na ufaulu wa wanafunzi wa shule hiyo ambapo alisisitiza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mpaka kukamilika kwa mradi huo.
“TEA tumefarijika sana kusikia Halmashauri imeshaanza kununua vitanda kwa ajili ya wanafunzi watakaoishi kwenye bweni hili pamoja na jengo kuwa katika hatua ya awali kabisa” Alimalizia Bi. Lupembe.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Afisa Elimu wa Wilaya ya Mkalama kwa upande wa shule za Msingi, Chacha Kehogo alisema kuwa halmashauri imejipanga vizuri kuupokea mradi huo mara utakapokamilika ambapo mpaka sasa tayari imeshanunua vitanda 31 ambavyo vimeshafika katika shule hiyo vikisubiri kukamilika kwa bweni.
“ Kwa hiyo niwahakikisheni TEA kuwa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama itaendelea kuunga mkono jitihada mlizozionesha ili na sisi tuoneshe tunachoweza kufanya na hata wadau wengine wakitaka kuja wasituone tegemezi hivyo niwashukuru sana na naomba msisite kututembelea tena kwa sababu bado tuna changamoto nyingi sana katka shule zetu hasa upande wa miundombinu. ” Alimalizia Kehogo
Mbali na mradi huo TEA imekamilisha ujenzi wa nyumba bora kabisa na ya kisasa ya walimu iliyopo katika kijiji cha Isanzu yenye thamani ya shilingi milioni 148 ambapo jumla ya Walimu tisa wa shule ya Sekondari ya Isanzu wanatarajia kuanza kuishi hapo muda wowote kuanzia sasa.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.