Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imepokea Tani Ishirini na Tano (25) ya Ruzuku ya Mbegu ya Alizeti aina ya Record C1 kutoka Serikalini itakayouzwa kwa bei ya Shillingi Elfu Kumi (10,000) kwa mfuko mmoja wa kilogram mbili kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wenye tija wa zao hilo Wilayani hapa.
Akiongea wakati akipokea Ruzuku hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo alisema kuwa Halmashauri imepokea Ruzuku hiyo kutoka kwa wadau wa kilimo ASA ambao waliahidi kutoa mbegu kwa wakulima.
‘’Ninawatangazia wakulima wa Wilaya ya Mkalama kuwa leo tumepokea Tani Ishirini na tano (25) za Mbegu za alizeti niwashukuru wadau wa kilimo ASA kutimiza ahadi hii iliyokuwa kiu ya wananchi kwa siku nyingi kupata mbegu iliyo bora’’ Alisema Mhe. Kizigo.
Aidha, aliongeza kuwa Wilaya ya Mkalama inatarajia kulima Hekta Elfu Arobaini na Nane (48,000) za Alizeti ikiwa zitahitaji takribani Tani 100 hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka ASA kuwa tayari wakati wowote pindi watakapohitaji kuongeza mbegu hizo ili kutosheleza mahitaji ya wakulima.
Sambamba na hayo, Mhe. Kizigo aliiomba Serikali kuharakisha Ruzuku ya Mbolea kwani msimu wa Mvua umeanza na wakulima wanasubiri kwa hamu kuhakikisha wanalima kilimo cha kisasa kitakachokuza pato lao binafsi na uchumi Wilayani hapa.
Akitoa shukrani zake kwa Ruzuku ya Mbegu ya Alizeti, Mtendaji wa Kata ya Nduguti Bw. Waziri Waziri aliishukuru Serikali kupitia wadau wa Kilimo ASA kutoa mbegu hizo ambazo zitawafikia Wakulima Wilayani Mkalama na kusema kuwa watahakikisha wanaunga Mkono Serikali kuzalisha zao hili kwa wingi kwani ni miongoni mwa Mazao ya kimkakati Mkoani Singida.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.