Balozi wa zao la Pamba Nchini na Mkuu wa Mkoa Mstaafu Mhe. Agrey Mwanry leo amehitimisha ziara yake ya kuhamasisha kilimo cha zao hilo kwa siku tatu Wilayani hapa katika kijiji cha Ilongo na na Igengu Kata ya Ibaga na kijiji cha Mpambala na Nyahaa Kata ya Mpambala.
Akiongea na wakulima wa maeneo hayo aliendelea kuwasisitiza wakulima kufuata mbinu bora za kilimo cha pamba ambazo zimefanyiwa utafiti kutoka Taasisi ya TARI na bodi ya Pamba kushirikiana na Nchi ya Brazil ambao ulibaini pamba ikilimwa vizuri itapelekea Mkulima wa wilaya ya Mkalama kupata Kg. 2500 kwa hekari kama ilivyo kwa Nchi za Agentina , Angola , Buknafaso pamoja na Misri.
Katika mafunzo hayo aliwataka wananchi kuandaa shamba mapema na kulitifua pia kuacha Ardhi ipumue hadi majani yaanze kuota ndipo waanze kukatia na kuweka mbegu ili kuufanya udongo kupoa na kupumua.
Hata hivyo aliendelea kuwasisitiza Wakulima kuhusu matumizi ya mbolea ya Samadi katika zao hilo ambapo aliongeza kuwa mbolea ya Samadi ina uwezo wa kutunza unyevu nyevu kwa muda mrefu ambao utasaidia zao la pamba kustawi vizuri.
‘’Mbolea ya samadi ni nzuri sana katika kilimo cha pamba kwasababu tunaweza kuipata majumbani mwetu ukisafisha banda la Kuku, wakinamama wakizoa majivu tayari hiyo ni mbolea ambayo hauhitaji gharama kubwa kuipata’’ aliongeza Balozi Mwanry.
’’ Serikali imeamua kuniteua kuwa balozi wa pamba Tanzania ulishawahi kusikia balozi wa matikiti au mchicha? sio kwamba imelenga kujifurahisha bali kukuza uzalishaji wa pamba nakuongeza tija katika zao hilo’’ Alisema Balozi Mwanry.
Aidha aliongeza kuwa kwa takribani miaka mitatu sasa uzalishaji wa zao la pamba ulishuka kutokana na mvua kuwa juu ya wastani kwa 2020/2021 na kuwa chini ya wastani kwa mwaka 2021/2022 ambapo .
‘’Uzalishaji wa zao hili halihitaji mvua kubwa kulizalisha bali inahitaji mvua ya kawaida sana kwa asilimia 50 tu kama mnavyojua Nchi ya Misri ni jangwa lakini ndio NChi pekee inayozalisha pamba nzuri na yenye ubora wa hali ya juu’’. Alisisitiza Balozi Mwanry.
Pamoja na hayo alikutana na wakuu wa Idara na Vitengo wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama kufanya majumuisho ya siku tatu alizotumia katika wilaya ya Mkalama wakati akihamashisha zao hilo ambapo aliwataka Maafisa Kilimo, Maafisa Ugani pamoja na wataalamu wote kuwatembelea wakulima kila muda ili kujua maendeleo yao pamoja na changamoto zinazowakabili.
Sanjari na hayo , Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos alimhakikishia Balozi Mwanry kuwatembelea Wakulima pamoja na kuwashauri wananchi juu ya kilimo bora cha pamba na kusimamia kwa ukaribu ili kuwa na tija kwa zao hilo ambalo litapelekea pato la halmashauri kukua.
‘’sisi kama wilaya tutahakikisha tunawasapoti wakulima wadogo ili kuwa na tija ya uzalishaji katika zao hili’’ aliongeza Bi. Messos.
Paia alimshukuru Balozi wa pamba Tanzania kufika wilayani Mkalama na kuongea na wakulima ambapo alisema kama wilaya watahakikisha zao hilo linalimwa kwa wingi wilayani hapo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.