Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu kwa kujenga Madarasa ya kutosha kwa nchi nzima Ili kuhakikisha wanafunzi wakiume na wakike wanapata elimu iliyo bora kwa masilahi mapana ya nchi.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Diwani wa viti Maalumu Frolence Misaiy alipotaka kujua "Je, ni lini Serikali itajenga Daharia (Bweni) kwa Shule zote za Sekondari ili kuepuka mimba kwa watoto wa kike wanaotembea umbali mrefu kwenda shule na kukutana na vishawishi njiani?"
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kujenga Shule nyingi kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mapambano ya Uviko 19 na kuongeza kuwa changamoto ya Madarasa sasa imepungua hivyo kwa fedha zingine zinazotolewa na Serikali watafanya mpango wa kuendelea kujenga Daharia kwa Shule ili kuwezesha wanafunzi wa kike kusoma bila vishawishi na kutimiza ndoto zao.
Afisa elimu taaluma Sekondari Wilaya ya Mkalama Stephen Ludovick amesema kuwa wanaendelea kuwafuatilia wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na mimba hadi sasa ni wanafunzi nane (8) wamerudi Shule kwa hiari yao na zoezi hilo ni endelevu ili kuwabaini wanafunzi wote waliokatisha masomo yao ili waweze kurudi na kufikia malengo yao ya kupata elimu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama James Nkwega aliwasisitiza wataalamu wote kila mmoja Kwa nafasi yake kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ili kuharakisha Maendeleo ya Wilaya ya Mkalama .
Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki Francis Isack amesema kuwa akiwa kama mwakilishi wa wananchi atahakikisha anasimamia na kusemea bungeni mambo mbalimbali ikiwepo kuomba ajira kwa Walimu ili kuhakikisha Wilaya ya Mkalama inakua na Walimu wa kutosha na kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi Wilayani hapa huku akiomba kusitishwa kwa uhamisho kwa Walimu Wakuu wanaofaulisha vizuri Wanafunzi Ili kuendeleza ufaulu mzuri katika shule hizo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.