“Jana Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imepokea fedha kwa ajili ya kumalizia miundombinu yote ya Zahanati za Kidarafa, Milade na Nduguti hivyo muda si mrefu tutafungua Zahanati hizo na Wananchi wa maeneo hayo wataanza kupata huduma zote stahiki za kiafya”
Hiyo ni kauli iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga alipokuwa katika kijiji cha Kinyambuli kukagua ujenzi wa Kituo bora na cha Kisasa cha Afya Unaoendelea kijijini hapo.
Mradi huo unaogharimu kiasi cha Shilingi milioni 700 unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Aprili Mwaka huu ambapo jumla ya Shilingi milioni 400 zilipokelewa na Halmashauri ya Wilaya na Kuhamishiwa katika akaunti ya Serikali ya Kijiji hicho ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati.
“Shilingi Milioni 300 zilizobaki zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa ambapo tayari tumeshazielekeza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili pindi tu Kituo kitakapokamilika huduma ianze mara moja” Alisisitiza Sanga.
Sanga alibainisha faida kadhaa ambazo wananchi wa Wilaya ya Mkalama kwa ujumla watanufaika nazo baada ya kukamilika kwa kituo hicho ikiwa ni pamoja na kusogezewa karibu huduma muhimu na za lazima ikiwemo ile ya Kuhifadhi Maiti na Kufanya Upasuaji ambapo Wananchi wa Mkalama wanalazimika kwenda mpaka hospitali ya Hydorm kwa ajili ya kupata huduma hizo.
“Lakini pia ninapenda kuwajulisha kuwa katika mwaka ujao wa Fedha Halmashauri inakusudia kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo tayari eneo la kujenga hospitali hiyo limeshatengwa na kinachosubiriwa ni Fedha tu kwa ajili ya kuanza Utekelezaji wa Ujenzi wa Hospitali hiyo” Aliongezea Sanga.
Mpaka kufika mwezi Juni mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama inatarajiwa kupiga hatua kubwa katika sekta ya Afya baada ya kukamilika kwa wodi ya wazazi ya Zahanati ya Nduguti, Vifaa tiba na miundombinu yote katika zahanati ya Milade na Kidarafa na Ujenzi wa Majengo ya Chumba cha Upasuaji, wodi ya Wazazi, Maabara ya Kisasa, Chumba cha Kuhifadhia Maiti na Nyumba bora ya Watumishi wa kituo hicho.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.