Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Peter Serukamba amesema kuwa Serikali imejipanga kutatua kero za Wananchi kwenye masuala ya Miundombinu ya barabara , maji , Afya , umeme na Elimu ili kuhakikisha mwananchi anapata huduma hizo ipasavyo.
Mhe. Serukamba ameyasema hayo leo Februari 21, 2023 katika Kijiji cha Gumanga , Kata ya Gumanga Wilaya ya Mkalama wakati wa muendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero za Wananchi .
Mhe. Serukamba aliongeza kuwa kero zote walizoziwasilisha mbele yake zitatatuliwa na kushughulikiwa kwa wakati kabisa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
‘’Niwapongeze wananchi wa Kijiji cha Gumanga kujitokeza kwa wingi na kuja kuwasilisha changamoto zenu, nimefurahi kuona mna ari ya kuuliza maswali na kero zote mlizowasilisha ni za kutaka maendeleo, ninawahakikishia yote nimeyachukua na nitayafanyia kazi ‘’ Aliongeza Mhe. Serukamba
Kufuatia kero za miundombinu ya barabara Mhe. Serukamba alimuagiza Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini ( TARURA) kutembelea barabara ya Kinankamba , Ikungu mpaka Mkiko na ile ya njia panda ya Ikungu- Kinandili inayoenda Miganga ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanaunganishwa na mtandao wa barabara hizo ili waweze kupitisha mazao yao na kufanya shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato na kukuza uchumi.
Katika hatua nyingine Mhe. Serukamba amewataka watendaji wa Vijiji na Kata kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutatua kero za wananchi na kutenda haki ikiwa ni pamoja na kuacha kubagua wananchi kutokana na itikadi zao za dini au Chama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amesema kuwa kwa kushirikiana na vingozi wake watahakikisha wanatatua na kushughulikia kero zote za wananchi Wilayani Mkalama ikiambatana na ripoti na namna walivyotatua changamoto .
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama Bw. Lameck Itungi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida kuanzisha ziara ya kutembelea kila wilaya kwaajili ya kutatua changamoto hii inaonyesha Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa vizuri nakuahidi kuwa uongozi wa Chama Wilaya ya Mkalama wapo bega kwa bega kuunga mkono juhudi hizo.
Akiongea kwa niaba ya Wananchi , Diwani wa Kata ya Gumanga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. James Mkwega amesema wananchi wa Kata hiyo wamefurahi kuona Mkuu wa Mkoa anafika kwenye maeneo yao kusikiliza na kutatua changamoto zao ambapo aliahidi ushirikiano mkubwa katika kuunga mkono juhudi hizo ambapo pia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi wanaposikia mikutano ya namna hiyo ili kero zao zisikilizwe na kupatiwa ufumbuzi
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.