Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema serikali imejipanga kutatua kero zote za wananchi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora huku akiwataka watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kuwatumikia wananchi kwa kuwatembelea kwenye maeneo yao kusikiliza na kutatua kero zao.
Amesema hayo leo wakati wa ziara yake ya Kikazi aliyoifanya July 17 2022 wilayani Mkalama ambapo katika ziara hiyo alitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la mawe lilijengwa katika barabara ya Iguguno- Kikhonda- Kinampundu lenye urefu wa mita 30 na upana wa mita 7 katika kijiji Cha Lukomo lenye thamani ya sh Mill 102 pamoja na kuzindua ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mkalama iliogharimu kiasi cha sh Bill 1.33.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa aliongea na Wananchi wa Wilaya ya Mkalama na kusema kuwa Serikali ya awamu ya sita imekusudia kuleta maendeleo kwa wananchi ndio maana imekua ikitoa fedha nyingi kwaajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwataka kuunga mkono juhudi hizo kwa kufanya kazi kwa bidii.
Hata hivyo Mheshimiwa Majaliwa aliwapongeza Wahandisi wa wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kwa ujenzi wa daraja zuri na lenye ubora kwakutumia teknolojia rahisi ya mawe na kusema daraja hilo litakua mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Lukomo na wilaya kwa ujumla.
Alisema ipo haja ya wahandisi wengine kuiga taaluma hiyo ya mawe kwa kila Mkoa kwakua kila Mkoa una mawe mengi jambo ambalo litaweza kupunguza gharama za ujenzi na kuokoa fedha nyingi za serikali katika ujenzi huo.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa aliwapongeza wakala wa Majengo Tanzania TBA kwa kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa asilimia 100 na kuridhishwa na ubora wa Ofisi hiyo huku akisema kukamilika kwa ofisi hiyo utarahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wilayani hapo.
‘’wahandisi wetu wa TBA Tanzania sasa ninaweza kufungua, siwezi kufungua bila kukagua ,ndio sababu niliingia huko ndani kuona kama nyumba inatosha na ina viwango? na nyie mmeona viwangoee kwahiyo nimeridhika na viwango’’alisema Mheshimiwa Majaliwa.
Naibu waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi Festo Ndungange alisema serikali imetoa Bill 2.6 katika sekta ya Afya wilayani Mkalama kwaajili ya kujenga vituo vya afya, vifaa tiba , huduma za upasuaji huku akisema serikali imetoa Bill. 2.6 kwaajili ya kuboresha miundo mbinu ya elimu kwakukamilisha madarasa ya shule za msingi na Sekondari.
Pamoja na hayo Mh. Ndungange alisema serikali imeongeza bajeti ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tarura kutoka mill 600 hadi bill. 2 lengo ni kuunganisha barabara kupitika kwa urahisi ili kuchochea maendeleo ya wilaya, hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutunza miundombinu hiyo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.