Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge amewapongeza wananchi wa Kitongoji cha Gajaroda wilaya ya Mkalama kwa kuendelea kuwapa makarani wa sensa ya majaribio Ushirikiano katika kutekeza majukumu yao na kufanikisha zoezi hilo kwa 90%.
Ameyasema hayo Mapema leo katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kujionea namna zoezi la Sensa ya Majaribio linavyoendelea katika Kitongoji cha Gajaroda Kijiji cha Dominiki Kata ya Mwangeza wilaya ya Mkalama Mkoani Singida .
Aidha Dkt Mahenge amesema kuwa lengo la serikali ni kuwa na takwimu sahihi za wakazi wa maeneo husika ikijumuiya takwimu za watu , Makazi yao ,Mifugo pamoja na mali wanazomiliki ili kurahisisha mipango ya serikali pamoja na vipaumbele kwa kila eneo.
Katika hatua nyingine amewataka Viongozi mbalimbali kila mtu kwa nafasi yake kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa Sensa na kulipokea zoezi hilo kama fursa kwao kwa maendeleo yao na kwa Mkoa kwaujumla.
‘’lengo kubwa ni kuisaidia serikali kuwa na taarifa kamili ni nini kinafanyika kwenye maeneo yao na watu wanaoishi kule wanajishughulisha na nini itasaidia serikali kuwaingiza kwenye mipango ya maendeleo,pia tunapojua idadi ya Watoto au watu inaisaidia serikali kujua kuwa wapeleke huduma gani kwahiyo wananchi wakijitokeza kwa wingi ndio watakula keki kubwa yaTaifa’’ Ameongeza Dkt Mahenge RC Singida.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ,Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe.Sophia Kizigo amesema kuwa wananchi wamepokea zoezi hilo vizuri kwani walipewa hamasa kutoka kwa Kamisaa wa Sensa kitaifa Mhe.Anna Makinda huku akiomba kutatuliwa changamoto zilizojitokeza katika zoezi la Sensa ya majaribio ikiwa ni pamoja na uchache wa makarani pamoja na kuongeza siku kwaajili ya kuhoji Dodoso kuu la Sensa kutokana na umbali uliopo kutoka kaya moja hadi nyingine.
Elifrida Yunde ambaye ni karani wa zoezi la Sensa ya Majaribio Kitongoji cha Gajaroda amesema kuwa anawashukuru wananchi kwa usirikiano wanaoutoa kwao huku akiongeza kuwa pamoja na changamoto wanazozipata mpaka sasa zoezi hilo limefanikiwa kwa 90% ambapo pia ameiomba serikali kuboresha Dodoso kwa Sensa ya wat una Makazi ya mwaka 2022 kutokana na Dodoso la majaribio kuwa refu.
Baraka Joseph na Hilda Amsii ni miongoni mwa wananchi wa kitongoji cha Gajaroda ,wamesema kuwa sensa hii ya majaribio imeonyesha taswira nzuri ya Sensa ya mwaka 2022 ambapo wameahidi kutoa ushirikiano wakutosha kwa serikali pamoja na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajawa na mwamko kuhusu zoezi hili ili serikali iweze kupeleka huduma muhimu kama kama vile maji,umeme,Hospitali pamoja na shule.
Zoezi la Sensa ya majaribio lilianza Semptember 8 mwaka huu na linatarajiwa kukamilika September 19 mwaka huu .
Kauli mbiu ikiwa ni ‘’SENSA KWA MAENDELEO JIANDAE KUHESABIWA’’
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.