Rc Serukamba akipanda mti katika kampeni aliyoizindua Leo January 14 2023 wilayani Mkalama
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba amesema Serikali ya Mkoa wa Singida imejipanga kupanda Miti milioni tatu ili kurudisha uoto wa asili na kuufanya Mkoa kuwa wa kijani.
Amesema hayo mapema leo wakati akizindua zoezi la upandaji Miti Wilayani Mkalama iliyohusisha maeneo ya Njia panda , Barabara kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, maeneo ya chanzo cha maji Nduguti pamoja na Hospitali ya Wilaya.
Aidha, Mhe. Serukamba alitumia fursa hiyo kuongea na Viongozi pamoja na Wananchi wa Wilaya ya Mkalama na kuwapongeza kuendeleza zoezi la upandaji miti ambapo aliwataka kila mtu kuwa balozi mzuri wa mazingira na kuagiza kila mwananchi kupanda Miti minne kila nyumba kuhakikisha Mkalama inakuwa ya kijani ili kukabiliana na mabadiliko tabia ya nchi.
‘’Mkoa wa Singida tumejipanga kupanda Miti ya kutosha ipatayo milioni tatu na ili tufikie lengo hilo ni lazima kila Mwananchi apande Miti minne kwa kila kaya, tukipanda Miti Mkalama itavutia na kupendeza na kila mtu atavutiwa kuja kukaa Mkalama’’ Aliongeza Mhe. Serukamba.
Pamoja na hayo Mhe. Serukamba aliwashukuru Wananchi wa Wilaya ya Mkalama kujitokeza kwa wingi kupanda Miti, hivyo kuwataka kila mmoja kutunza na kuilinda Miti iliyopandwa tarehe 14/01/2023 ili iweze kuwaletea hewa safi pamoja kurejesha uoto wa asili kwa faida ya vizazi vya baadae.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama, Bi. Elizabeth Rwegasira aliwapongeza Watumishi wote wa Wilaya pamoja na Wananchi wa Nduguti , Maziliga na vijiji jirani kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kupanda Miti na kusisitiza kuwa zoezi hili ni endelevu na lilianza toka siku ya Uhuru na leo Miti Mia tano thelathini imepandwa na kuahidi usimamizi mzuri ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kurudisha uoto wa asili kila sehemu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama, Bw. Lameck Itungi pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. James Mkwega wamesema zoezi hili ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi na watahakikisha Wilaya inasimamia zoezi hili kikamilifu pamoja na kuwepo kwa Sheria zinazosimamia utunzaji wa Mazingira na kuweka utaratibu kila Kijiji kuwa na hifadhi ya Msitu.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.