RC SERUKAMBA AZINDUA MRADI WA UMWAGILIAJI WA BIL.34/-SKIMU YA MSINGI WILAYANI MKALAMA
MKUU wa Mkoa wa Singida,Mhe. Peter Serukamba, leo (Juni 14, 2023) amezindua Mradi wa Skimu ya umwagiliaji utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 34. 176 utakaotekelezwa katika Kijiji cha Msingi, Kata ya Msingi Wilayani Mkalama mkoani Singida.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, amesema Mradi wa Skimu ya Msingi utakuwa na jumla ya eneo la hekta 2,000.
Mhe Serukamba amesema mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wakazi 12,000 kutoka Vijiji vinne vya Ishinsi, Ndurumo, Msingi na Kidi vilivyopo Kata ya Msingi tarafa ya Kinyangiri ambao watalima mazao ya mpunga,mahindi na mbogamboga Kwa misimu miwili hadi mitatu kwa mwaka.
Ameongeza kwakusema kuwa shughuli kuu zitakazofanyika katika shughuli ya ujenzi wa mradi ni ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa Lita 1,875,000,ujenzi a mifereji ya umwagiliaji yenye kilometa 19.12, uchimbaji wa mifereji ya matupio yenye urefu wa kilo mita 42.539, uchimbaji wa mifereji ya kuingiza Maji mashamba yenye urefu wa jumla ya kilometa 34.778.
Shughuli nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za mashamba zenye urefu wa kilomita 36.1, kusawazisha ekari 2,000 za mashamba,ujenzi wa kilomita nane za barabara na makaravati sita kuelekea ndani ya mradi na ujenzi wa vigawa Maji 14,vipunguza mwendo,viumbo angalizi 90,vipitisha maji 90,makaravati 14 pamoja na vivuko nane.
Mhe .Serukamba amesema Ili mkandarasi aweze kuendelea na kazi za ujenzi bila kukwama Tume ya Umwagiliaji ihakikishe inamlipa mkandarasi kila anapokamilisha hatua mojawapo ya ujenzi.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la mradi aliwataka wananchi kutouza ardhi kwani lengo la Serikali ni kutaka wenyeji wanufaike na mradi huo.
Mhe. Serukamba aliwaondoa hofu wananchi kwamba watanyang'anywa ardhi kwamba hizo ni propaganda hakuna atakayenyang'anywa na kuagiza wenyeviti wa vijiji kusimamia kuhakikisha kila mwananchi anapata eneo la kulima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe.Moses Machali, ametuamia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huu kwani utasaidia kuinua uchumi wa wilaya ya Mkalama
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. James Mkwega, amesema fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mradi huu ni nyingi hivyo watahakikisha wanautunza mradi ili wanufaike na kubadili maisha ya Wananchi.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.