Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba ameutaka uongozi wa Wilaya ya Mkalama kuweka ratiba ya kutembelea Wananchi Vijijini kusikiliza kero zao pamoja na kutatua migogoro ya Ardhi ambayo inaoneka ni tatizo sugu Wilayani hapa.
Amesema hayo mapema leo January 18, 2023 wakati akisikiliza kero za wananchi Wilayani hapa ambapo pia aliagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kupitia Maafisa Ardhi kusimamia kurudisha Ardhi ya Edina Philipo Mkumbo na Melisiana Nelson Mnoma ambao wana mgogoro na Serikali ya Kijiji cha Yulansoni.
‘’mimi ni muumini wa haki na muumini wa kutatua kero za Wananchi hivyo ninawataka Wakuu wa Idara na Vitengo msikae ofisini wekeni ‘program’ ya kwenda Vijiji msikilize na kutatua changamoto za Wananchi na sio kuwaachia Serikali ya Kijiji, haiwezekani Serikali ya Kijiji ikabeba hatima ya Wananchi wa Mkalama.’’ Aliongeza Mhe. Serukamba.
Aidha, Mhe. Serukamba aliwataka Maafisa Ardhi kwenda kwa wananchi kupima Ardhi yao pamoja na kuwapatia Hati Miliki ili kuondoa migogoro inayotokana na Ardhi pamoja na kuwataka kutafuta jengo kwa ajili ya Baraza la Ardhi Wilaya ili wananchi waweze kusikilizwa mashauri yao Wilayani hapa na kuacha kufuata huduma hiyo Wilayani Iramba.
‘’Niwaombe Maafisa Ardhi kutafuta jengo kwa ajili ya Baraza la Ardhi Wilaya kama Mwenyekiti wa Baraza yupo mnasubiri nini kutoa huduma, tumieni hata Ukumbi wa Halmashauri siku ya Baraza ili wananchi wote wapate huduma Wilayani Mkalama kwani wengi hawana uwezo wa kwenda Iramba’’ alisisitiza Mhe. Serukamba.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Katibu Tawala Wilaya Bi. Elizabeth Rwegasira amemshukuru Mkuu wa Mkoa kufanya ziara Wilayani hapa pamoja na kusikiliza kero, hivyo kuahidi kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa pamoja na kuwasilisha ripoti ya namna walivyoshughulikia na kutatua kero za Wananchi.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.