
Na Pius Maganga
Katibu Tawala Wilaya ya Mkalama, Bi. Happyness Sulle, amewataka wananchi wa wilaya hapa kuzingatia matumizi ya teknolojia na ushauri wa kitaalamu katika shughuli za kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija uzalishaji mazao
Bi. Sulle alitoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama wakati akizungumza na wakulima katika kongamano la ufunguzi wa msimu wa kilimo 2025/26 lililofanyika tarehe 18-11-2025 katika Kijiji cha Maziliga wilayani hapa.
“Katika msimu huu wa 2025/2026 tuzingatie teknolojia zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo. Ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan amehakikisha Maafisa Ugani wanapatikana hadi kwenye kata ili usihangaike kwenda wilayani kutafuta huduma. Huduma zimeletwa hadi mlangoni, ni juu yako mkulima kuitumia,” alisema Bi. Happiness.
Aidha, aliwataka Maafisa Ugani kutekeleza majukumu yao kikamilifu, ikiwemo kuitisha vikao, kutoa elimu, na kusimamia kikamilifu shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo yao.

Akihitimisha hotuba yake, Bi. Happyness ameipongeza Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kazi nzuri wanayoifanya, ikiwemo utekelezaji wa chanjo kwa mifugo na kuwataka wananchi kuhakikisha wanatoa mifugo yao kwa ajili ya chanjo.
Hafla hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya, ambapo wameshiriki kupata elimu kupitia mabanda ya maonyesho kuhusu kilimo cha kisasa, afya ya udongo, matumizi ya mbegu bora, pamoja na ushauri wa njia stahiki za kuongeza tija katika kilimo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.