Mkoa wa Singida kupitia Wilaya ya Mkalama na mkoa wa Manyara kupitia wilaya ya Mbulu leo wameadhimisha tamasha la pamoja la utamaduni wa makabila makuu yaliyopo kwenye mikoa hiyo tukio lililofanyika katika kijiji cha Hydorm.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa utamaduni na Michezo Bi. Suzan Mlawi ambaye alizipongeza wilaya hizo kwa kufanikisha maadhimisho ya tamasha hilo huku akisisitiza kuwa suala la kudumisha mila na utamaduni wa watanzania ni jukumu la kila mwananchi.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na taifa lililokufa hivyo ni lazima kila mmoja wetu aenzi na kudumisha mila na desturi zetu kwani ndio kitambulisho chetu hata tunapokuwa nje ya nchi yetu” Alisisitiza Bi. Mlawi.
Bi Mlawi aliongeza kuwa maadhimisho hayo ni ishara kubwa inayoonesha ushirikiano wa dhati uliopo baina ya Wilaya ya Mkalama na Mbulu ambapo aliwasihi viongozi wa pande hizo mbili kuendeleza na kudumisha umoja huo huku wakiendelea kuenzi mila na desturi za Mtanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliipongeza kamati ya maandalizi ya tamasha hilo na kuwataka wananchi wote wa Wilaya ya Mkalama kuhakikisha wanajitokeza kwenye tamasha hilo ambalo litafanyika kila mwaka.
“Kuhudhuria tamasha hili ni utalii tosha kabisa na mtu anaweza kuja na familia yake kwa ajili ya mapumziko hivyo nawasihi wananchi wa Mkalama na maeneo mengine ya jirani wafike kushuhudia tukio hili la asili kabisa” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Tamasha hilo lilipambwa na burudani mbalimbali za asili kutoka makabila ya Wagogo, Wasukuma, Wangoni, Wahadzabe, Wanyiramba, Wanyisanzu, Wairaqi, Wamasai na Wadatoga huku kivutio kikubwa kikiwa ni vipaji vilivyooneshwa na mbunge wa jimbo la Mbulu vijijini Mhe. Flatei Massay na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ambao walionesha ustadi mkubwa katika kucheza ngoma na nyimbo za asili.
Mbali na ngoma na nyimbo za asili kutoka katika makabila tofauti, tamasha hilo lilijumuisha pia maonesho ya vitu mbalimbali vya asili, wanyamapori kama vile Simba, Chui, Mamba na kobe mwenye umri wa miaka 200 na utamaduni wa kabila la wadatoga.
Kijiji cha Hydorm kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Mkalama na Mbulu kwa sasa kinatambulika kama kitovu cha Afrika kutokana na kujumuisha makundi makuu manne ya jamii za bara la Afrika ambao ni Wanyiramba na Wanyisanzu (Wabantu), Wadatoga (Wanailo), Wahadzabe (Wakwesa) na Wairaqi (Wakushi).
Makundi hayo pamoja na kuishi pamoja kama ndugu katika kijijichi hicho wanatofautiana katika lugha, historia, utamaduni na mgao wa utumiaji wa rasilimali.
Miongoni mwa wadhamini wakubwa wa tamasha hilo kwa mwaka huu ni pamoja na serikali ya Norway chini ya kitengo cha Utamaduni kinachojulikana kama 4CCP (4 Corners Cultural Programs), Mbuga ya wanyama ya Ngorongoro, Kampuni ya Yara, Shirika la bima ya afya la MHI na benki ya CRDB.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.